Tanzania inatarajia
kuokoa mabilioni ya fedha kutokana na kuanza kutekeleza mfumo wa uagizaji
mafuta kwa pamoja na kwa kiasi kikubwa.
Hayo yalibainishwa Dar es
Salaam jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage alipofungua
programu ya mafunzo maalumu ya wajasiriamali wanaoagiza nishati ya mafuta,
yaliyoandaliwa na First National Bank (FNB).
Mafunzo hayo yanahusu
namna ambavyo wagizaji mafuta, wanaweza kupata dhamana za benki na kulipa kwa
pamoja mara moja, tofauti na sasa ambapo wanaagiza kwa pamoja, lakini kila
mwagizaji analipa kivyake.
Akizungumza katika
mafunzo hayo, Mwijage alisema mfumo wa siku za nyuma ambao waagizaji hao mafuta
hawakuwa na ushirikiano, ulikuwa na usumbufu na ulikuwa unalipozea taifa zaidi
ya dola za Marekani milioni 60 (Sh bilioni 102) kila mwaka.
Hivi sasa waagizaji hao,
wanaagiza kwa pamoja kupitia mfumo huo mpya, ambao umepunguza gharama,
umeongeza tija na ufanisi na kuokoa muda na rasilimali nyingine.
Hata hivyo, alisema taifa
linaweza kuokoa fedha zaidi, endapo watakuwa na mfumo wa kulipa kwa pamoja.
Alisema pamoja na mfumo
mpya kupunguza gharama kwa waagizaji umekuwa na manufaa kwa watumiaji, ambao
ndio wadau wakubwa katika biashara hiyo.
Mkurugenzi wa Umoja wa
Waagizaji Mafuta (PIC), Michael Mjinja alisema changamoto kubwa ilikuwa ni
gharama za usafirishaji mafuta kwa meli lakini sasa changamoto hiyo haipo tena
na vile vile waagizaji wanaaminiwa zaidi kwenye masoko.
No comments:
Post a Comment