WANAFUNZI 10,000 KUJIUNGA SEKONDARI AWAMU YA PILI

Wanafunzi  9,824 waliohitimu elimu ya msingi mwaka jana katika mkoa wa Dar es Salaam, wanatarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari katika awamu ya pili ya uchaguzi.

Mkuu wa Mkoa huo, Saidi Meck Sadiki alisema kuwa katika uchaguzi wa awamu ya kwanza, wanafunzi 36,610 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule mbalimbali za mkoa huo.
“Tunawahakikishia wazazi na wanafunzi kwamba hatutawaacha wanafunzi hao waliofaulu waingie mitaani bali tunapambana kuhakikisha wanaingia katika uchaguzi wa awamu ya pili,” alisema.
Aidha Sadiki alisema wamefanikiwa kwa asilimia 100 kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete la kujenga maabara tatu za sayansi katika shule zote za sekondari, lengo likiwa ni kukuza somo la sayansi nchini.
“Tayari tumeshajenga maabara mpya 281 za kemia, fizikia na bayolojia na kwa sasa tunakamilisha miundombinu ya mifumo ya gesi na maji katika maabara hizo ili tuwe na maabara za kisasa,” alisema.
Alisema kwa kukamilisha agizo hilo anaamini kwamba watoto watapendelea kusoma masomo hayo kwa sababu ya kuwepo kwa miundombinu na kufanya mazoezi ya vitendo tofauti na ilivyokuwa mwanzo.
Hata hivyo, alisema mkoa kwa kushirikiana na Manispaa zake wamejipanga kuhakikisha ufaulu wa darasa la saba unapanda kila mwaka ambapo kwa mwaka jana wanafunzi walifaulu kwa asilimia 78 kutoka 75 ya mwaka juzi.

No comments: