WABUNGE WAOMBA WANAUME WAFUNGWE KIZAZI

Wabunge wametaka kuwepo na udhibiti wa ongezeko la watu nchini kwa  kutaka wanaume wadhitibiwe katika uzazi, kama ilivyo kwa wanawake huku wengine wakitaka serikali kuboresha rasilimali bila kudhibiti uzazi.

Miongoni mwa waliotaka wanaume wafungwe kizazi kama inavyofanyika kwa wanawake ni Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki, Celina Kombani ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Wakichangia mada katika semina ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 kwa wabunge, iliyoandaliwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) walisema ni vyema kuwa makini katika kudhibiti uzazi, kwani inaweza kusababisha athari za baadaye kuwa na wazee wengi kuliko vijana.
Mbunge wa Dole, Sylvester Mabumba (CCM) alisema hakuna haja ya kuogopa kuongezeka kwa watu, bali rasilimali zitumike vizuri kwa kutunga sheria maalumu ya kubana mafisadi kwa kuwafilisi.
Mbunge wa Arumeru Magharibi, God ole Medeye alishauri kuwa si vyema kudhibiti uzazi, kwani kuna nchi walifanya hivyo sasa wamebaki na wazee tu hivyo ni vyema kuangalia hali ya uchumi na uzazi.
Kombani alisema kumekuwa na suala la uzazi wa mpango kwa wanawake tu, hivyo katika kudhibiti idadi ya watu ni vyema wanaume nao wakadhibitiwa kwa kufungwa uzazi.
Alisema ikiwa familia inataka kudhibiti kuzaa ni vizuri mwanamke akifunga kizazi na mwanamume naye afunge kuzaa.
Huku akiungwa mkono na Mbunge wa  Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM) aliyesema ni vyema kudhibiti wanaume katika uzazi kwa  kuwa na idadi sawa kati ya wanawake na wanaume.
Mbunge  wa Rungwe Magharibi, Profesa David Mwakyusa alisema kuwadhibiti wanaume ni jambo la muhimu, kwani iwapo mwanamume atakuwa amechepuka mara 100 atazaa watoto 100, lakini mwanamke akichepuka mara 100 atazaa mtoto mmoja.
Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) alisema kudhibiti kuzaa ni kupinga vitabu vya dini vilivyosema kuzaana sana kwani kila mtoto anakuja kwa riziki yake huku akibainisha wazi kuwa ana watoto 12 na anatarajia kufikisha 20 kwani kuna faida wapo wenye uwezo tofauti.
Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alisema ni vyema kuangalia mifano ya Japan na Norway na pengine walipodhibiti uzazi na sasa wanaona athari yake, hivyo ni vyema kuwaachia wataalamu kupata uwiano wa  kuzaa idadi ya watoto wanaotakiwa kuzaliwa.
Akihitimisha majadiliano hayo, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema tatizo la ongezeko la watu nchini ni kubwa na lazima kujipanga kudhibiti uzazi, kwani itapunguza masuala mbalimbali.
Alisema ukizaa watoto wachache ni lazima mke na watoto kuwa na afya njema huku huduma za elimu na afya kuwa njema, kwani hata China walidhibiti uzazi na sasa wanalegeza masharti baada ya kuona matunda yake, kwani ardhi haiongezeki bali watu wanaongezeka.
Akifungua semina hiyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitaka wabunge kuhakikisha ongezeko la watu nchini, linaendana  na ukuaji wa uchumi wa asilimia 7 kwa muongo mmoja.
Alitaka  kuhimiza matumizi bora ya uzazi wa mpango katika kaya, Sera ya Idadi ya Watu na Makazi mwaka 2006 haina budi katika suala la ongezeko la watu.
Alisema hayo katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta    na kusema idadi ya watu nchini imeongezeka kutoka watu milioni 34.4 mwaka 2002 hadi milioni 44.9 mwaka 2012. Alisema watu wengi Tanzania ni watoto ambao ni asilimia 43 ya Watanzania wote wenye umri chini ya miaka mitano.

No comments: