RUSHWA YATIMUA KAZI 400 MIZANI, MAGUFULI ASEMA HUO NI MWANZO TU

Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli amevitaka vyombo vya dola kuingilia kati suala la rushwa kwenye vituo vya mizani za kupimia uzito wa magari yanayosafirisha mizigo, akisema rushwa hiyo imekithiri.

Magufuli alitoa agizo hilo alipotembelea na kukagua kituo cha mizani cha Mpemba wilayani Momba, ambapo alipita kituoni hapo kwa kushtukiza, alipokuwa katika ziara yake ya kukagua barabara akielekea wilayani Ileje.
Kupita kwa Magufuli kwenye mizani hiyo, kulitokana na yeye kujionea namna barabara ya kati ya Mbeya na Tunduma ilivyoharibiwa, kutokana na malori yanayosafirisha mizigo inayozidi uzito unaotakiwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda mpaka wa Tunduma kabla ya kuvushwa kuelekea nchi jirani.
Baada ya kufika kituoni hapo, alihoji maofisa waliokuwa zamu ni kwa nini barabara ionekane kuharibika upande mmoja wa magari yanayotoka Mbeya kwenda Tunduma badala ya pande zote mbili.
Maofisa hao walimweleza kuwa kuharibika kwa upande huo wa barabara, kunatokana na malori kutoka Mbeya kwenda Tunduma, kutopimwa uzito kwakuwa hakuna mizani nyingine kabla ya kufika kituoni hapo.
Hata hivyo, majibu ya maofisa hayo hayakumridhisha waziri huyo na ndipo akatupia lawama utendaji kazi wa maofisa wa vituo vya mizani, akisema umekithiri kwa kupokea rushwa.
Alisema licha ya serikali kuwafukuza kazi watumishi 400 wa idara hiyo mwaka jana na kuajiri upya, bado tatizo la upokeaji rushwa kwa watumishi waliopo ni kubwa mno.
“Mwaka jana tuliamua kuwafukuza kazi watumishi 400 waliokuwepo kwa kuwa tuliona wamejikita katika rushwa badala ya kutimiza majukumu yao. Hapo tukaajiri watu walio na elimu nzuri tukijua tumetibu tatizo. Lakini bado rushwa inaendelea. Matokeo yake barabara zetu zinaendelea kuharibika,” alisema.
“Watumishi wa vituo vya mizani ni mabilionea wakubwa. Hii yote ni kwa kuwa wanapokea rushwa kutoka kwa watu wanaosafirisha mizigo iliyozidi uzito na kuharibu barabara zetu,” alisisitiza.
Alisema ni wakati sasa kwa vyombo vya dola, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) na Idara ya Upelelezi ndani ya Jeshi la Polisi, kufanya uchunguzi kwa maofisa wa vituo vya mizani nchini.
Alisema iwapo vyombo hivyo vitalifanyia kazi suala hilo, visisite kuchukua hatua stahiki kwa watumishi watakaobainika na kuzitaka pia ofisi za makatibu tawala wa mikoa, kufuatilia suala hilo.

No comments: