UTAFITI WAWAPATIA VIJANA USHINDI WA KISHINDO URAIS 2015

Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Elimu (TEDRO), limesema katika utafiti walioufanya kuhusu ushiriki wa vijana katika siasa na matarajio kuelekea uchaguzi mkuu 2015, umeonesha kwamba endapo mgombea urais kijana atapendekezwa atakubalika kwa asilimia 82.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa shirika hilo, Jacob Kateri alisema katika wananchi hao waliohojiwa pia asilimia 11 walisema vijana hawatakubalika na asilimia saba walisema hawajui.
Alisema utafiti huo umeandaliwa na kufanyika Tanzania Bara na maeneo yaliyohusishwa ni kanda za kijiografia ili kuwezesha uhusishwaji mpana wa Watanzania na katika kila wilaya wamehojiwa wananchi wa vijiji vitatu kwa kuzingatia siasa za eneo husika.
Aidha alisema utafiti huo umeonesha sababu mbalimbali zinazoweza kuwa kichocheo cha vijana kuingia katika siasa ambapo zilizochukua uzito ni uzalendo kwa asilimia 67 ambapo wananchi walisema vijana wengi wameingia katika siasa kwa sababu ya uzalendo.
“Sababu nyingine ni kimbilio baada ya kukosa ajira kwa asilimia 57, uwezo mdogo wa watangulizi wao katika nafasi husika kwa asilimia 60, mafanikio ya wanasiasa vijana walio mahiri asilimia 72, vyama vya siasa kuwapa nafasi vijana katika vyama vyao kwa asilimia 59 na kukubalika kwa vijana kwa asilimia 63,” alisema.
Aidha alisema wanasiasa vijana waliopendekezwa kupitia chama tawala aliyeoonekana kuongoza kwa kukubalika ni Mwigulu Nchemba kwa asilimia 38, Dk Emmanuel Nchimbi kwa asilimia 26, January Makamba kwa asilimia 24, William Ngeleja kwa asilimia 11 na Lazaro Nyalandu kwa asilimia 10.
Wengine ni Hamisi Kigwangala kwa asilimia saba, Deo Filikunjombe kwa asilimia tano, Esther Bulaya kwa asilimia 2 na waliosema hakuna anayefaa walikuwa asilimia 9 na asilimia 13 walipendekeza wengine wasio vijana.
Utafiti huo pia unaonesha kwamba kijana anayepewa nafasi kubwa endapo atasimamishwa kupitia upinzani anayeongoza  ni Zitto Kabwe kwa asilimia 18, James Mbatia kwa asilimia 16, Tundu Lissu kwa asilimia 14, Halima Mdee kwa asilimia nne na David Kafulila kwa asilimia sita.
Wengine ni Julius Mtatiro kwa asilimia nne, John Mnyika kwa asilimia saba, Joshua Nassari kwa asilimia mbili, Moses Machali kwa asilimia nne na asilimia 11 ya wananchi walisema hawajui na asilimia 16 walisema hawaoni anayefaa.
Hata hivyo, utafiti huo ulionesha kwamba endapo wakishindanishwa vijana wote bila kujali itikadi zao anayeongoza  kwa kukubalika ni Mwigulu Nchemba kwa asilimia 27, Zitto Kabwe kwa asilimia 19, January Makamba kwa asilimia 14, James Mbatia kwa asilimia 11 na Emmanuel Nchimbi kwa asilimia nane.
Wengine ni Lazaro Nyalandu kwa asilimia saba, Tundu Lissu kwa asilimia tano, Hamis Kigwangala kwa asilimia nne, wengine waliotajwa wasio vijana ni asilimia nne na wasiofaa walikuwa ni asilimia mbili.
Mapema Mkurugenzi wa Mafunzo wa Utafiti wa TEDRO, Jackson Coy alisema utafiti huo wameufanya bila shinikizo kutoka kwa mtu yeyote na waliufanya kuhusu siasa kutokana na kwamba mwaka huu utafanyika uchaguzi mkuu.
Alisema lengo la utafiti huo limechambua ushiriki wa vijana katika siasa kama wagombea, mchango wa wanasiasa vijana katika kufuatia misingi ya utawala bora na uwajibikaji, utekelezaji wa ahadi za wagombea kwa wapiga kura na matarajio ya wananchi kwa vijana katika kuelekea uchaguzi mkuu.
“Utafiti tunaoendesha ni mwendelezo wa uchambuzi wa changamoto za elimu, ndani ya dira ya TEDRO na programu ya mchango wa elimu katika kufungua fursa za ajira, siasa ikiwa ni mojawapo ya fursa zenye kimbilio la vijana,” alisema.
Hadi sasa TEDRO inaendesha utafiti wa Mitandao ya Kijamii inavyoathiri wanafunzi wa sekondari na kutazama njia rafiki katika kutumia mitandao hiyo kama njia ya kujifunzia na kuendeleza sekta nzima ya elimu.
Utafiti huu uliotarajiwa kuhusisha wilaya 24 Tanzania Bara, umeendeshwa katika wilaya 18, kila wilaya ikiwa imewakilishwa na wahojiwa 45 waliochaguliwa 15 kutoka kila kijiji; hivyo utafiti huu kuhusisha vijiji 54 kwa ujumla.
Wilaya ambapo utafiti umefanyika ni Njombe Mjini, Ludewa, Mbeya Mjini, Kilwa, Lindi Mjini, Mtwara Mjini, Morogoro Mjini, Kisarawe, Kinondoni, Tanga Mjini, Vunjo, Arumeru, Singida, Kasulu, Kigoma Mjini, Bukoba Vijijini, Biharamulo na Mwanza Mjini (Nyamagana).
Katika utafiti huu uliohusisha watu 910, taarifa binafsi za wahojiwa zilizokusanywa ni pamoja na zile zinazohusu umri wa wahojiwa, jinsia, hali ya ndoa, kazi, kiwango cha elimu na vyama vya siasa vinavyoongoza majimbo sehemu uchaguzi ulipofanyika. 
Lakini wakati matokeo hayo ya utafiti yakianikwa, kwa upande wa CCM, Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni akiwa mjini Songea, Ruvuma alikokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 38 ya chama hicho, alisema chama chake bado hakina mgombea mpaka sasa.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kuwashawishi wanaoonekana kuwa na uwezo wa kuongoza huku wakiwa hawana 'madoa’ waweze kujitosa katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.

No comments: