SHERIA MPYA YA VIBALI VYA AJIRA YAJA

Wizara ya Kazi na Ajira iko  katika mchakato wa kuandaa Sheria mpya ya utoaji wa vibali vya ajira kwa wageni ili kudhibiti kuajiriwa kwa wageni ili kufanya kazi ambazo Watanzania wenyewe wanaweza kuzifanya.

Alisema mchakato huo uko karibu kukamilika na utapelekwa bungeni kutokana na ratiba na kueleza kuwa itasaidia kudhibiti wafanyakazi wageni wanaoingia nchini bila utaratibu maalum na kusababisha kuajiliwa kwenye kazi ambazo wenyeji wanaweza kufanya.
Waziri katika wizara hiyo, Gaudentia Kabaka aliliambia Bunge kuwa sheria hiyo itatoa mwongozo juu ya utoaji vibali, kwani sasa kumekuwa na sehemu nyingi hivyo kuwa na sehemu moja pamoja na adhabu kwa wageni wanaofanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.
Alisema hivi karibuni walibaini wageni 300 walioingia nchini kufanya kazi katika kiwanda cha saruji cha Dangote, Mtwara kwa kazi zinazoweza kufanywa na watanzania.
Wakati huo huo, wafanyakazi zaidi ya 350 wa Kampuni ya mgodi wa Bulyanhulu waliodai kuachishwa kazi baada ya kupata madhara wakiwa kazini wametakiwa kwenda kwenye  Wakala wa Usalama na Afya  Mahali pa Kazi (OSHA)  kupimwa ili kuthibitisha iwapo walipata madhara hayo kutokana na kazi walizokuwa wakifanya ili kuweza kutibiwa.
Alisema kuwa OSHA ndiyo wenye mamlaka ya kuthibitisha kuwa wafanyakazi hao wameathirika na kwa  utaratibu walitakiwa kupeleka OSHA barua kutoka kwa mwajiri ili kuweza kupimwa na kujua athari walizopata wakiwa kazini lakini tangu wafukuzwe kazi mwaka 2007 hawakupeleka barua hiyo.
“Tumegundua kuwa wafanyakazi hao hawakuwa na uhusiano mzuri na chama cha wafanyakazi hivyo kusababisha ufuatiliaji wa suala hilo kuwa mgumu hivyo ninawaagiza kwenda OSHA Dar es Salaam wakapime kwani wako tayari wao pamoja na wengine 50 waliofukuzwa “alisema Kabaka.
Pia alitaka chama cha wafanyakazi migodini (TAMICO) kuwaunganisha wafanyakazi hao ili kufuatilia kwa pamoja na kuepusha kuwa mmoja mmoja.
Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jafo (CCM) alisema wafanyakazi hao wamekuwa wakihangaika katika ofisi mbalimbali ikiwemo kwenye Wizara ya Kazi na Ajira kufuatilia suala hilo.

No comments: