ULINZI MKALI KESI YA WAFUASI WA UAMSHO


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, iliimarisha ulinzi wakati kesi ya ugaidi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Shekhe Farid Hadi Ahmed na wenzake ilipotajwa.

Askari walikuwa wengi katika eneo la Mahakama huku kila mtu aliyeingia getini akikaguliwa  kwa kifaa maalumu na kupapaswa ili kuangalia kama ana silaha.
Jana kesi hiyo ilitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda na kuahirishwa hadi Machi 4 mwaka huu itakapotajwa tena.
Wakili wa Serikali, Peter Njike alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini bado wanasubiri uamuzi wa rufaa waliyoikata katika Mahakama ya Rufani.
Upande wa Jamhuri ulikata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ulioamuru Mahakama ya Kisutu kusikiliza na kutolea uamuzi hoja za washitakiwa.
Washitakiwa wanadaiwa kati ya Januari mwaka jana na Juni mwaka huu katika maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikula njama ya kutenda kosa kwa kutafuta watu wa kushiriki vitendo vya ugaidi.
Katika mashitaka mengine, wote wanadaiwa katika kipindi hicho, huku wakijua ni kosa walikubaliana kuwaingiza nchini, Sadick Absaloum na Farah Omary washiriki vitendo vya ugaidi.

No comments: