MKUU WA WILAYA MUFINDI APANDISHWA KIZIMBANI KWA RUSHWA


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewapandisha mahakamani Mkuu wa  Wilaya ya Mufindi,  Evarista Kalalu na wakurugenzi wawili kwa makosa mawili yanayohusiana na rushwa kinyume na Kifungu cha 32 cha Sheria ya Takukuru Namba 11 ya mwaka 2007.

Katika kesi hiyo inayowaunganisha maofisa wengine wawili wa halmashauri ya  wilaya ya Mufindi,  wanatuhumiwa kuisababishia halmashauri hasara ya Sh milioni 3.
Kesi hiyo iliyopewa jina la kesi ya  uhujumu uchumi namba moja ya mwaka 2015,
ilifunguliwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Mufindi mkoani hapa.
Mkuu wa wilaya hiyo na watuhumiwa hao wengine kwa pamoja wamekana mashitaka yao mbele ya Hakimu  Mfawidhi wa mahakama hiyo, Victoria Nongwa.
Watuhumiwa wengine katika shitaka hilo ni  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mikindani mkoani Mtwara, Limbakisye Shimwela ambaye wakati kosa hilo likitendeka kati ya Desemba 2010 na Februari 2011, alikuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi na mwingine ni  Mkurugenzi wa halmashauri ya Biharamulo mkoani Kagera, Nasibu Bakari.
Watuhumiwa wengine waliofikishwa katika mahakama hiyo, kutokana na ushiriki wao wa makosa katika kesi hiyo ni Ofisa  Mipango wa Halmashauri ya Mufindi, Cosmas Mduda na Fundi Ujenzi wa wilaya hiyo, Fedrick Zaveri.
Akisoma shitaka linalowakabili watuhumiwa hao mahakamani hapo, Mwendesha mashitaka wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Imani Mizizi alidai mbele ya Hakimu   Mfawidhi wa mahakama hiyo kuwa kati ya Desemba 2010 na Februari 2011 watuhumiwa hao kwa pamoja walikula njama ya  kutenda kosa la rushwa kinyume na kifungu cha 32 Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Katika kosa la pili, linalowakabili watuhumiwa watatu katika kesi hiyo, ambao
ni Shimwela ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtwara/Mikindani, Bakari ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo na Cosmas ambaye ni fundi ujenzi, ni lile la matumizi mabaya ya ofisi kinyume na kifungu cha 31 cha sheria kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kati ya Desemba 2010 na Februari 2011, watuhumiwa  hao watatu walitumia ofisi vibaya kwa kuingia mkataba na Fedrick Zaveri kwa ajili ya ujenzi wa vyoo, bafu za kuogea na mfumo wa maji katika shule ya sekondari ya Ihalimba bila kufuata Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka  2004.
Ilidaiwa kuwa kutokana na hatua hiyo, watuhumiwa waliisababishia hasara ya Sh  milioni tatu  Halmashauri ya  Wilaya ya Mufindi.
Watuhumiwa wote wamekana kosa na kuachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya kila mmoja kuwa na wadhamini wawili na bondi ya Sh  milioni moja kwa kila mdhamini.
Hakimu  Victoria aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 13 mwaka huu, watu hao watakapokuja kusomewa maelezo ya awali.

No comments: