NEC YATAMBIA BVR, UANDIKISHAJI WAPIGAKURA KUANZA FEBRUARI 23


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema katika majaribio ya uandikishaji wananchi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, mfumo mpya wa uandikishaji wa 'Biometric Voter Registration Kit' (BVR), umefanikiwa kwa asilimia kubwa licha ya changamoto kadhaa, na ina uhakika mfumo huo utatumika kuwaandikisha Watanzania wote katika daftari hilo bila matatizo. 

Aidha, Tume hiyo imebadilisha tarehe ya kuanza rasmi uandikishaji wa wananchi katika daftari la kudumu uliokuwa uanze Februari 16, katika mkoa wa Njombe, hadi Februari 23, mwaka huu, ili kutoa nafasi kwa wadau kuweza kujiandaa vyema. 
Pamoja na hayo, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, wameonesha wasiwasi juu ya utaratibu mzima wa uandikishaji wananchi katika daftari la kudumu kupitia BVR, kuwa kama utafanyika na kumalizika kwa wakati, kutokana na tume hiyo kuchelewa kufanya mambo mengi, ikiwemo elimu ya uraia na kutoa ratiba ya uandikishaji. 
Akifungua mkutano ulioandaliwa na tume hiyo kwa ajili ya kukutana na vyama vya siasa kujadili uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Damian Lubuva, alisema tume hiyo ilianza utaratibu wa majaribio ya uandikishaji kwa kutumia mfumo huo katika mikoa mitatu ambayo ni Dar es Salaam, Morogoro na Katavi. 
“Kwa ujumla uandikishaji ulifanyika vizuri na kwa mafanikio katika maeneo yote, idadi ya watu walioandikishwa pia katika maeneo hayo iliongezeka na kuvuka lengo ambalo tume iliweka kwa zaidi ya asilimia 100 licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa, hii ni dalili nzuri kwamba mfumo huu utafanikiwa,” alisema Jaji Lubuva. 
Alisema tume hiyo katika eneo la Kawe mkoani Dar es Salaam ililenga kuandikisha wananchi 14,312, lakini waliandikishwa wananchi 15,123 sawa na asilimia 105.67, Kilombero mkoani Morogoro waliandikishwa wananchi 19,188 wakati lengo la Tume lilikuwa wananchi 17,290 sawa na asilimia 110.9. 
“Pia katika mkoa wa Katavi, wilayani Mlele, tuliweka lengo la kuandikisha wananchi 11,104 lakini kupitia mfumo huu wa BVR ambao katika kila kituo tulitumia BVR kit 80, tuliandikisha wananchi 11,210,” alisisitiza. 
Aliwahakikishia wanasiasa hao kuwa, kutokana na majaribio ya mfumo huo katika mikoa hiyo, pamoja na kubaini changamoto kadhaa, tume hiyo ina uhakika mfumo huo ni imara na unaweza kutumika kuandikishia Watanzania wote katika muda uliopangwa bila matatizo. 
Hata hivyo, alisema tume hiyo imebadilisha muda wa kuanza uandikishaji kutoka Februari 16 hadi 23, mwaka huu, ambapo katika mkoa wa Njombe pekee wanatarajia kutumia vifaa vya BVR takribani 250 huku vifaa vingine 7,050 vikisubiriwa kuwasili nchini kwa ajili ya uandikishaji kuendelea maeneo mengine. 
“Suala la ratiba tunalifahamu na tutaitoa muda wowote, tayari Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya vifaa hivi ambavyo vinatokea China, awamu ya kwanza vifaa takribani 2,000 vitawasili wiki ya kwanza ya mwezi Machi, napenda nitoe wasiwasi, Tume iko huru, wazi na haina chochote inachokificha wala kutumika na mtu,” alisema. 
Aidha, Jaji Lubuva, alisema kutokana na taarifa za sensa, tume hiyo imeongeza vituo vya uandikishaji wapiga kura kutoka vituo 24,919 vya zamani hadi vituo 36,109.
Naye Mkurugenzi wa tume hiyo, Julius Malaba, alisema katika majaribio ya mfumo huo wa BVR, changamoto kadhaa zilijitokeza ikiwemo mfumo mzima wa BVR ulivyoandaliwa (setting), hardware na programu zinazotumiwa na mfumo huo pamoja na maeneo ya uendeshaji uandikishaji huo. 
 “Changamoto zote hizi tumezifanyia kazi kwa kuzirekebisha. Katika BVR zitakazotumika mkoani Njombe nazo zimefanyiwa marekebisho kutokana na changamoto zilizojitokeza, ila tumechukua tahadhari za uhakika ili kuhakikisha utaratibu mzima unafanyika bila tatizo,” alisema Malaba. 
Wakitoa maoni yao kuhusu mada hiyo, wengi wa viongozi wa vyama vya siasa walionesha wasiwasi na kutokuwa na imani na tume hiyo kwa kushindwa kuwasilisha ratiba nzima ya uandikishwaji nchi nzima ikiwa ni pamoja na utaratibu huo kuanza huku vifaa vingi vikiwa bado havijawasili. 
Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, alisema bado kuna masuala mengi yenye utata ambayo tume hiyo haijayafafanua likiwemo suala la programu zipi zinazotumiwa na mfumo huo, lini vifaa vyote vitawasili na kwanini mpaka sasa hakuna ratiba ya uandikishwaji wapiga kura. 
“Tunaomba ratiba kamili ya uandikishwaji, mnasema mmeongeza muda ili tujipange na kutoa mawakala, sasa tutajipangaje wakati hata hatujui ratiba yenyewe, lakini pia bado elimu ya uraia iliyotolewa hasa juu ya BVR kwa wananchi na watendaji watakaoendesha uandikishaji haitoshi, tuna wasiwasi, naomba jambo hili baadaye lisivuruge nchi,” alisisitiza Mwenyekiti wa CUF Profesa Lipumba. 
Hata hivyo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliitaka NEC kutokukaa kimya na kujibu hoja mbalimbali zinazojitokeza ili kuondoa utata na dhana potofu zinazosambazwa na baadhi ya watu kuhusu mfumo huo ambazo endapo hazitojibiwa kiuhakika wananchi huziamini.
“Kuweni wawazi, msichoke kuwafafanulia watu na kumbukeni kuwa zoezi hili ni muhimu lisipofanyika vizuri tunaweza kujuta mambo yakiharibika.
“Nasema hivi kwa kuwa siku zote mambo yakiharibika au uongo ukisambazwa na kuaminiwa bila majibu, lawama zote huiangukia CCM,” alihadharisha. 
Akijibu changamoto zilizotolewa na viongozi wa vyama vya siasa, Lubuva alisema watazifanyia kazi, huku akiongeza kuwa suala la ratiba itatolewa hivi karibuni, lakini akadokeza kuwa, baada ya uandikishaji kuanza Njombe, itafuatia mikoa mingine huku Zanzibar na Dar es Salaam zitakuwa za mwisho.

No comments: