Kesi inayomkabili
kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini Shehe Ponda Issa Ponda jana
imeahirishwa hadi Februari 16, mwaka huu kwa mashahidi wa upande wa
mashitaka kuendelea kutoa ushahidi mahakamani.
Tayari mashahidi saba wa
upande huo wameshatoa ushahidi wao mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa
Morogoro, akiwemo aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Faustine Shilogile.
Akiongozwa na
Wakili Mkuu Mwandamizi Serikali, Benard Kongola alieleza jana mbele ya
Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo , kuwa siku hiyo alikuwa na mashahidi
wawili badala ya watatu ambapo mmoja alishindwa kufika mahakamani
kutokana na kupatwa na udhuru.
Mashahidi ambao
wameshatoa ushahidi wao mbali na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa,
ni aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Morogoro (OCD), Sadick Tindwa,
ambaye kwa sasa ni OCD Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga.
Shahidi mwingine
ni mtaalamu wa kitengo maalumu cha uchunguzi wa picha Sajini taji
Aristides, ambaye aliwasilisha ushahidi wake juzi kwa kuleta mkanda wa video
unaodaiwa kuonesha uhalisia wa tukio zima la kesi yake inayomkabili ya
kutoa maneno ya uchochezi.
Mrakibu Mwandamizi wa
Polisi, Japhet Mabeyo ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya Uchunguzi Makao
Mkuu wa Upelelezi Dar es Salaam, alikuwa ni shahidi wa sita jana kutoa ushahidi
wake mahakamani hapo.
Katika ushahidi wake
akiongozwa na Wakili wa Serikali , Mabeyo alieleza majukumu yake akiwa
Mkuu wa Kitengo cha Maabara ni kusimamia masuala ya utawala ya kila siku
ikizingatiwa kitengo hicho kinashughulika na mambo mbalimbali yakiwemo kutoka mikoani.
Shahidi wa saba katika
kesi hiyo ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Utambuzi Polisi Mkoa wa Morogoro
Inspekta wa Polisi Jafert Msongole, alitoa ushahidi wake kwa kueleza taratibu
alizozifanya katika kuchukua mkanda wa video iliyoonesha namna mshitakiwa
alivyotoa maneno ya uchochezi katika kongamano la Eid Pili lililofanyika Agosti
10, mwaka 2013 katika viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege Manispaa ya
Morogoro.
Aliendelea kuieleza
Mahakama kuwa uchukuaji wa picha za matukio mbalimbali ni utaratibu wa kitengo
hicho na kwamba alimtuma askari wake kwenda kuchukua picha kwa kuwa tayari
alishapata taarifa kuwa huenda Shehe Ponda angehudhuria katika kongamano hilo.
Hata hivyo upande wa
utetezi ukiongozwa na wakili Juma Nasoro ulimuuliza maswali ya msingi shahidi
huyo likiwemo la kutaka kujua kama kuwepo kwa Shehe Ponda katika kongamano hilo
kungevuruga amani.
Akijibu maswali hayo
Shahidi kuyo alieleza kuwa aliamini kuwepo kwa Sheikh Ponda katika kongamano
hilo kungeweza kuvuruga amani kwani alishapata taarifa kutoka kwa wakubwa wake
wa kazi kuwa Shehe Ponda hakutakiwa kuwepo katika kongamano hilo.
No comments:
Post a Comment