Kesi ya kumdhuru mfanyakazi wa ndani inayomkabili raia wa
Ufaransa, Folkertsma Laurent (41), imeahirishwa hadi Machi 31, mwaka huu
kutokana na shahidi kutofika mahakamani.
Awali, Wakili wa Serikali, Felista Mosha wa Mahakama ya
Wilaya ya Ilala, alidai kwamba kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa
na kwamba shahidi waliyemtegemea mahakamani hapo hakufika.
Pia alidai kuwa shahidi huyo alipewa onyo afike mahakamani
hapo ili kuendelea na ushahidi huo lakini hakufanya hivyo na kwamba hakutoa
taarifa.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassani aliahirisha kesi hiyo
hadi Machi 31, mwaka huu upande wa Jamhuri utakapoendelea kusikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alidai kuwa Wakili
anayemuwakilisha alipatwa na msiba hivyo alisafiri lakini mpaka anafika
mahakamani hakujua kama amesharudi au la.
Ilidaiwa Mei 23,
mwaka huu, maeneo ya Tabata Liwiti Wilaya ya Ilala, Laurent alimpiga na
kumsukuma Aneth Mponzi na kumsababishia maumivu mwilini. Mshitakiwa yupo nje
kwa dhamana.
No comments:
Post a Comment