HUU NDIO UTETEZI WA TIBAIJUKA NA CHENGE BARAZA LA MAADILI YA VIONGOZI


Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, limemsomea rasmi mashitaka aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, na kubainisha kuwa kiongozi huyo anastahili kujibu mashitaka kwa kosa la kuomba na kujipatia fedha kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Hata hivyo, Profesa Tibaijuka alikana mashitaka hayo, na kusisitiza kuwa hakukiuka maadili hayo ya viongozi wa umma, kwa kuwa fedha hizo hakuziomba kwa maslahi yake binafsi, bali kwa ajili ya kuendeleza na kuboresha taasisi yake inayotoa huduma ya elimu kwa watoto wa kike wasio na uwezo lakini wenye vipaji.
Akimsomea mashitaka hayo mbele ya baraza hilo, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wemaeli Mtei alisema Profesa Tibaijuka ambaye ni kiongozi wa umma, alishawishi na kuomba fedha na baadaye kupokea Sh bilioni 1.6 kutoka kwa James Rugemalira na mkewe.
Aidha, Sekretarieti hiyo kupitia shahidi wake ambaye ni Katibu Msaidizi wa Idara ya Viongozi wa Siasa kutoka Sekretarieti hiyo, Waziri Kipacha, alisema kupitia Kamati ya Uchunguzi iliyoundwa na sekretarieti kufuatilia sakata hilo, ilibaini kiongozi huyo aliomba na kupokea fedha hizo kupitia barua aliyoandika Februari 4, mwaka 2012.
“Tulibaini kuwa fedha alizoomba mlalamikiwa zilitumwa kwake kupitia akaunti yake namba 00120102640201 ya Benki ya Mkombozi iliyopo St Joseph jijini Dar es Salaam,” alisema huku akikabidhi baraza hilo barua hiyo ya Tibaijuka ya kuomba fedha na taarifa za kibenki kama ushahidi.
Alisema pamoja na hayo, kamati hiyo pia katika uchunguzi wake ilibaini mlalamikiwa ni mmoja wa wadhamini katika Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya  Barbro Johansson Girls Education Trust, ambapo barua kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), ilithibitisha suala hilo. Na kwamba wamiliki wa shule hiyo ndiyo wadhamini.
“Tumebaini kuwa mlalamikiwa alipokea kiasi hicho cha fedha na wadhifa aliokuwa nao kama Waziri, jambo lililomwingiza katika mgongano wa kimaslahi,” alisema.
Alisema kitendo cha mlalamikiwa kupokea fedha hizo na kuingizwa katika akaunti yake binafsi, ni kosa kwa mujibu wa masharti ya maadili ya viongozi wa umma kwa kuwa viongozi wa umma hawaruhusiwi kuomba fedha au msaada au kujipatia maslahi ya kiuchumi au kumpatia mtu mwingine maslahi hayo ya kiuchumi.
Wakili wa Tibaijuka, Dk Rugemeleza Nshara, alidai mbele ya Baraza mteja wake hakuna kosa alilofanya, bali alitumia wadhifa alionao kama viongozi wengine akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuomba na kuchangisha fedha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na si binafsi.
“Nataka kuuliza Baraza hili, ina maana juzi Waziri Mkuu, alivyoongoza uchangishaji fedha kwa ajili ya maendeleo alikwenda kinyume na maadili ya uongozi?,” alihoji.
Profesa Tibaijuka, alikiri kuomba fedha hizo kwa ajili ya kuendeleza taasisi hiyo yenye lengo la kujenga shule za mfano za wasichana wenyewe vipaji kila kanda ili kukuza na kuimarisha elimu ya mtoto wa kike nchini.
“Huu si msaada wa kwanza, tumekuwa tukifadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia msaada tuliopatiwa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, ambaye alitambua juhudi zetu na kutuunga mkono,  tumechangiwa na taasisi za ndani na nje na watu binafsi, kiasi kinachohitajika kuboresha shule hizi ni dola za Marekani milioni 14 sawa na takribani Shilingi bilioni 25.2,” alisema.
Alisema pamoja na Rugemalira aliyetoa Sh bilioni 1.6, pia mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi alichangia taasisi hiyo Sh milioni 278, ikiwemo Serikali ya Sweden iliyomaliza mkataba wake iliyochangia Sh bilioni 8.1.
“Sisi tuliopo kwenye taasisi hii, tunaaminiana na ni waadilifu ndiyo maana fedha nilizoomba ziliingizwa kweli kwenye akaunti yangu lakini niliziwasilisha, zilizobaki ni deni nililokuwa naidai taasisi, lakini pia nimekopa Benki M Sh bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha taasisi hii na kuweka dhamana nyumba yangu iliyopo Oysterbay. Mbona hili hamlioni?,” alihoji.
Wakati akijitetea,  Tibaijuka aliomba akabidhi andiko lake mbele ya baraza hilo. “Nina andiko langu na naomba nilikabidhi, kabla hujafa hujaumbika, nasimama hapa leo kwa sababu tayari nimeshahukumiwa bila kusikilizwa, niliomba hata bungeni nipewe nafasi lakini nilihukumiwa kama Waziri nikavuliwa madaraka, nashangaa leo nimesimamishwa hapa kama mbunge,” alisema.
Alisema "mimi mpaka sasa nasema sijakiuka maadili labda wanasheria wanieleweshe kwa sababu nilisimama kama mimi wakati wa kuomba fedha na si kama waziri au mbunge, hivyo sasa naona lengo ni kunivunja moyo, kunidhalilisha, kunifanya kama mwanamke mhuni na tapeli.”
Aliendelea kujitetea, "nimekuja kujieleza ila.. Mimi siyo mwanasheria ila ukweli sina kosa na ndiyo maana nyaraka zote ambazo zipo hapa, mimi ndo nimewapa, nimekuja hapa kwa nia njema na naamini kwamba Baraza hili litanisikiliza kwa sababu ukweli ndiyo mwanzo wa maadili, lazima tupiganie haki na tupiganie ukweli.
"Kama mimi nimefanya kosa kusimama kuwasaidia watoto wenye vipaji ni kosa,  naomba mwanasheria anieleweshe na naomba ukweli usimame maana tukienda na fitina peke yake, hatutafika. Mimi ni profesa na mchumi na ni mstaafu wa muda mrefu na nina pensheni, sina makuu, maisha yangu ni 'simple' (ya kawaida) huwezi kunikuta Dubai... Ila nipo tunafanya maendeleo na wananchi wangu,” alisema.
Hata hivyo alisema fedha anazodaiwa kuhamisha baada ya kupokea na kukatwa za kulipa deni la Benki M, zilizobaki zilikuwa ni halali yake kwa kuwa alikuwa akidai shule hivyo fedha hizo zilizobaki ni kwa ajili ya matumizi yake binafsi.
"Mimi ni mchakarikaji, mtafuta fedha na kiongozi anayeshindwa kutafuta fedha kwa ajili ya watu wake hafai. Hivyo nilipolipwa milioni 117 (Shilingi), nilitoa milioni mbili nikachangia Kanisa la Makongo na nikatoa laki nne nikapeleka kanisani na milioni 10 niliitoa kwa ajili ya matumizi yangu ya kununulia mboga, "  alisema.
Shahidi wa Profesa Tibaijuka ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi hiyo, Balozi Paul Rupia katika ushahidi wake mbele ya Baraza, alisema fedha hizo zimetafutwa na Profesa Tibaijuka.
Alisema aliitaarifu bodi kwamba zipo fedha zimeingia katika akaunti yake na zinatakiwa kulipa madeni wanayodaiwa.
Alisema katika kikao hicho cha kutoa uamuzi wa kugawanywa kwa fedha hizo kilichofanyika Luguruni , hakuhudhuria, ingawa alikuwa na taarifa zote  za kinachoendelea.
Rupia alisema bodi hiyo haikumpa masharti yoyote  Profesa Tibaijuka ya kumaliza kulipa madeni hayo kwa sababu hawakuona sababu ya kumfuatilia kwa kuwa walimwamini, kutokana na juhudi zake binafsi za kupata fedha hizo.
Shauri hilo lilianza saa 3 na baadaye kuahirishwa kwa muda hadi saa 6.30 mchana, lilipoanza kusikilizwa tena na  kumalizika saa  11.45 jioni.
Katika shauri hilo, Profesa Tibaijuka alitoa ushahidi kwa zaidi ya saa tatu, akilalamika kuonewa na kuhukumiwa bila kusikilizwa.
Shauri hilo liliahirishwa hadi Machi 13 mwaka huu,  kutokana na muda kutotosha. Wakili aliomba udhuru wa kwenda Marekani kwa siku 10 na Jaji Msumi alikubali.
Jaji Msumi alisema wajumbe watapitia shauri hilo na siku hiyo itaamuliwa, endapo hukumu  itatolewa wazi au kwa uamuzi wa ndani.
Shahidi wa Profesa Tibaijuka ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi hiyo, Balozi Paul Rupia katika ushahidi wake mbele ya Baraza, alisema fedha hizo zimetafutwa na Profesa Tibaijuka.
Alisema aliitaarifu bodi kwamba zipo fedha zimeingia katika akaunti yake na zinatakiwa kulipa madeni wanayodaiwa.
Alisema katika kikao hicho cha kutoa uamuzi wa kugawanywa kwa fedha hizo kilichofanyika Luguruni , hakuhudhuria, ingawa alikuwa na taarifa zote  za kinachoendelea.
Rupia alisema bodi hiyo haikumpa masharti yoyote  Profesa Tibaijuka ya kumaliza kulipa madeni hayo kwa sababu hawakuona sababu ya kumfuatilia kwa kuwa walimwamini, kutokana na juhudi zake binafsi za kupata fedha hizo.
Shauri hilo lilianza saa 3 na baadaye kuahirishwa kwa muda hadi saa 6.30 mchana, lilipoanza kusikilizwa tena na  kumalizika saa  11.45 jioni.
Katika shauri hilo, Profesa Tibaijuka alitoa ushahidi kwa zaidi ya saa tatu, akilalamika kuonewa na kuhukumiwa bila kusikilizwa.
Shauri hilo liliahirishwa hadi Machi 13 mwaka huu,  kutokana na muda kutotosha. Wakili aliomba udhuru wa kwenda Marekani kwa siku 10 na Jaji Msumi alikubali.
Jaji Msumi alisema wajumbe watapitia shauri hilo na siku hiyo itaamuliwa, endapo hukumu  itatolewa wazi au kwa uamuzi wa ndani.

…Chenge akwama
Mbunge wa Bariadi Magharibi,  Andrew Chenge ameendelea kupambana ili Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, lisiendelee kusikiliza shauri lake, licha ya pingamizi lake kutupiliwa mbali jana.
Chenge amewasilisha ombi la kukata rufaa Mahakama Kuu dhidi ya uamuzi wa baraza hilo, uliotolewa jana na kusomwa na Jaji Hamisi Msumi, ukisema madai yaliyowasilishwa kwenye pingamizi la mbunge huyo, hayalihusu baraza hivyo shauri linapaswa kuendelea kusikilizwa kama ilivyopangwa.
“Tumeliangalia kwa makini pingamizi hili (la Chenge) na kuipitia amri ya Mahakama Kuu inayozuia suala la akaunti ya  Escrow kujadiliwa na tumejiridhisha kuwa, Baraza hili halihusiani na orodha ya watu waliotajwa kwenye amri hiyo waliyowekewa pingamizi,” alisema Jaji Msumi.
Alisema baraza hilo limebaini katika amri hiyo, yako makundi yaliyotajwa kutojihusisha na suala hilo hadi pale Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi katika kesi ya msingi na katika makundi hayo, Baraza hilo la Maadili halikutajwa.
Alisema pia pingamizi kubwa, lililowekwa katika amri hiyo ni kuzuia kupelekwa bungeni na kujadiliwa kwa taarifa ya ukaguzi maalumu wa miamala ya Escrow na masuala ya umiliki wa IPTL.
“Hivyo basi, Baraza limeona hoja iliyowasilishwa na kukabidhiwa na mlalamikiwa haina msingi, hivyo imekataliwa,” alisema Jaji Msumi.
Baada ya uamuzi huo, Chenge aliomba kuwasilisha hoja yake ya kukata rufaa akisema, “sina nia ya kubishana, ila nataka kuwasilisha nia ya kukata rufaa kwenda Mahakama Kuu, kupinga uamuzi huu wa Baraza ili suala hili litolewe uamuzi upya”.
Alisema anashangazwa na wanasheria wa baraza hilo, ambao hawajatumia muda wao ipasavyo kwa kwenda masjala ya Mahakama Kuu na kupitia amri hiyo ya Mahakama Kuu na kujiridhisha, kwa kuwa amri hiyo iko wazi, pana na imegusa maeneo mengi kuliko inavyofikiriwa.
“Naomba nitumie haki yangu ya kukata rufaa na kwenda Mahakama Kuu, naomba nipatiwe mwenendo mzima wa kesi, sasa sijui Baraza hili lina utaratibu wa kukata rufaa au mimi ndio nitalitambulisha suala hili kwa mara ya kwanza,” alihoji Chenge.
Kwa upande wake, Jaji Msumi alisema baraza hilo limemruhusu mbunge huyo ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akate rufaa dhidi ya uamuzi wa baraza hilo Mahakama Kuu, jambo litakalosaidia pia kuweka historia ya kisheria.
“Ni vyema tuachie Mahakama Kuu ambacho ni chombo cha juu kuliko Baraza hili, ili itueleze kama ni sahihi sisi kuendelea na shauri hili au la, kwa sasa sina uhakika kama kanuni zimetengwa kuhusu masuala ya rufaa kwenye Baraza hili,” alisema.
Alisema endapo Mahakama Kuu itaamua baraza hilo lisiendelee kusikiliza shauri hilo, shauri hilo halitasikilizwa, lakini ikiamuru liendelee, litaendelea kumhoji Chenge na kesi yake ya kukiuka maadili ya uongozi wa umma.
Juzi Chenge alisomewa rasmi mashitaka yanayomkabili na Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Hassan Mayunga, ambayo ni pamoja na kutumia madaraka yake vibaya alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kushauri Serikali iingie mkataba wa miaka 20 na kampuni ya IPTL.
Aidha, anadaiwa baada ya kustaafu wadhifa huo wa uanasheria mkuu wa Serikali Desemba 24, mwaka 2005, mwaka 2006 aliingia mkataba wa kuwa mshauri mwelekezi wa kampuni wa VIP Engineering and Marketing Limited iliyokuwa na hisa za asilimia 30 kwenye kampuni ya IPTL.
Lakini, pia mwanasheria huyo anadaiwa na baraza hilo, kuingia mkataba na kampuni ya VIP, uliompatia manufaa ya kifedha ya Sh bilioni 1.6 kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na fedha hizo ziliingizwa Februari 5, mwaka jana katika akaunti ya mlalamikiwa namba 00120102523901, iliyopo kwenye Benki ya Mkombozi  Tawi la St Joseph  jijini Dar es Salaam.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo juzi, mbunge huyo alikataa kesi hiyo kusikilizwa na kuwasilisha pingamizi hilo la kutaka suala hilo kutoendelea kusikilizwa kwa kuwa tayari kuna kesi ya msingi Mahakama Kuu inayoendelea kusikilizwa.

No comments: