KAMPUNI YA KUSAMBAZA MABATI YAFUNGIWA DAR


Kampuni ya usambazaji na uuzaji mabati Afrika Mashariki, Uni Metal East Africa Limited ya Dar es Salaam, imezuiwa isiuze wala kusambaza mabati, kwa muda usiojulikana, kwa sababu hayana ubora.

Sambamba na kukataza mabati hayo yasiuzwe, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limefunga ghala la kampuni hiyo, lenye mabati ya geji 30 na 32, yaliyoingizwa kutoka India yakiwa hayana viwango vya ubora vinavyotakiwa, kuruhusu hatua zaidi zichukuliwe kulinda yasipenyezwe sokoni.
Ofisa viwango wa shirika hilo, Sirili Kimario alisema muda mfupi kabla ya kufunga ghala hilo kuwa, wakala wa ukaguzi wa viwango vya ubora wa bidhaa kutoka nje ya Tanzania, Bureau Veritas, anayefanya kazi kwa niaba ya TBS nchini India ndiye aliyeruhusu mabati hayo yaingizwe nchini wakati hayakidhi matakwa ya viwango vya ubora.
"Baada ya kufanya uchunguzi wetu kwa bidhaa mbalimbali zilizoingizwa kutoka nje, tumebaini kuwa zipo zilizoruhusiwa na mawakala wetu ziingizwe na kupewa hati ya kukidhi viwango vya ubora, ilhali hazina, ni hafifu," Kimario alisema na kuongeza:
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Rohit Panjwani alisema wamejipanga kuanza taratibu za kumshitaki mshirika huyo wa TBS kutoka India kwa kuwa amewasababishia hasara isiyopungua Sh bilioni tano, kwa kuruhusu waingiza  mzigo ambao baadaye umeonekana haufai kwa kutokidhi viwango vya ubora.
Alisema: "Hii si haki kwa sababu, tulifuata taratibu zote za kuthibitisha ubora wa mabati haya kabla ya kuruhusiwa kuyanunua na kuyasafirisha kuja Tanzania, mwaka mmoja uliopita.
“Endapo wakala Bureau Veritus angetueleza kuwa sampuli ile tuliyoipeleka haifai tusingeyasafirisha kwa gharama kubwa hivi (Sh bilioni 5) na wala Watanzania walionunua kuanzia mwaka wote uliopita wasingeyanunua".
"...Tunachukua hatua ya kumshitaki wakala huyo wa India. Na TBS nayo inapaswa imfuatilie na kumchunguza kwa karibu kuthibitisha uzuri au uovu wake, ili mambo kama haya yasitokee tena".

No comments: