Hukumu kuhusu ni familia
ipi inayostahili kuuzika mwili wa mwanamke Esther Hoseya unaogombaniwa na
familia mbili, itatolewa Jumatatu.
Hii ni baada ya Mahakama
ya Wilaya ya Bunda kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa wazee wa kimila wa pande hizo
mbili walioitwa kutoa ushahidi kukinzana.
Kutokana na hali hiyo,
Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Said Hamadi Kasonso, ameiahirisha kesi
hiyo hadi kesho, ili aweze kupitia ushahidi huo na kutoa hukumu ya kesi hiyo
vizuri itakayoamua familia inayostahili kuuzika mwili wa mwanamke huyo.
Mahakama hiyo juzi
ililazimika kuzuia mwili wa Esther aliyefariki dunia Februari 3, mwaka huu,
jijini Dar es Salaam, usizikwe na upande wowote, baada ya kutokea mgogoro wa
pande mbili wa kugombania mwili huo, akiwemo baba mzazi wa mwanamke huyo.
Familia hizo mbili ni
kati ya baba yake mzazi, Samwel Obinja, mkazi wa wilayani Rorya na Benard Odila
mkazi wa mjini Bunda, anayedai kuwa alikuwa tayari amekwishamuoa mwanamke huyo,
baada ya mume wake wa awali, Hoseya Daud, kufariki dunia mwaka 2005, jijini Dar
es Salaam.
Baada ya mwanamume huyo
kufariki, Odila anayedai kuwa ni mke wake, kwa sababu alikuwa akiishi naye Dar
es Salaam, alijitokeza na kuchukua mwili wa marehemu na kuusafirisha hadi
wilayani Bunda kwa ajili ya mazishi.
Wakati wakiandaa
shughuli za kuuaga mwili wa marehemu nyumbani kwake mjini Bunda, baba wa
mwanamke huyo, Obinja alikimbilia katika Mahakama ya wilaya ya Bunda na
kuwasilisha hati ya dharura yenye kiapo kwa ajili ya kupinga hatua hiyo.
Kutokana na hali hiyo
Hakimu Kasonso alimtuma karani wa mahakama hiyo, Nyawaye Jogo, kupeleka hati
yenye hoja kumi kuzuia mazishi hayo mpaka maamuzi ya mahakama hiyo
yatakapotolewa na kwamba wakikaidi amri hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Hakimu Kasonso jana
aliisikiliza kesi hiyo kwa kushirikisha wazee wa kimila wa kabila la Wajaluo,
kwa sababu ndoa ya awali ya mwanamke huyo ilifungwa kimila mwaka 1987.
Hata hivyo, ushahidi wa
kimila wa pande zote mbili uliotolewa na wazee wa kabila hilo ulipingana na
ndipo hakimu Kasonso akaiahirisha kesi hiyo namba 3 ya mwaka huu, hadi kesho,
ili aweze kutoa hukumu hiyo.
No comments:
Post a Comment