Yanga imeanza vema michuano
ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuifunga BDF X1 ya Botswana mabao 2-0
katika mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya michuano hiyo.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga ijiweke kwenye
mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mechi ya marudiano itakayofanyika
baada ya wiki mbili mjini Gaborone, Botswana.
Mchezaji wa zamani wa Simba, Amis Tambwe ndiye
aliyekuwa shujaa wa Yanga baada ya kuifungia mabao yote mawili.
Tambwe alifunga bao la kwanza katika dakika
kwanza ya mchezo huo kwa kichwa baada ya kuruka juu na kuuwahi mpira wa kona
katikati ya mabeki wa BDF.
Katika kipindi hicho cha kwanza, BDF walionekana
kucheza kwa kujilinda zaidi hali iliyomaanisha kwamba walikusudia kupata sare.
Tambwe aliipatia Yanga bao la pili katika dakika
ya 56 akifunga tena kwa kichwa hatua tatu kutoka lango la BDF. Alifunga bao hilo
baada ya kuunganisha pasi safi ya Mrisho Ngassa aliyewachanganya mabeki wa BDF.
Kwa ujumla Yanga ilianza mechi hiyo kwa kasi
kiasi cha kuipoteza BDF XI katika dakika
20 za kwanza kabla haijakaa sawa na kujaribu kufanya mashambulizi.
Washambuliaji wa Yanga mara kadhaa walifika
langoni mwa BDF lakini walikosa umakini
na kujikuta wakipiga juu ama kupiga michomo dhaifu iliyodakwa na kipa wa
wapinzani wao.
Katika dakika 20 za mwanzo BDF XI ilifanya
shambulizi moja la nguvu wakati Master Mastara alipoingia eneo la hatari,
lakini alipiga shuti lililopaa juu.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kushambulia
kwa kasi, huku BDF XI wakionekana kupoteza muda zaidi kwa kuhitaji matokeo
yabaki kama yalivyo na hapo ndipo Tambwe alipowapachika bao la pili.
Dakika ya 64, 65 na 67 lango la BDF XI lilikuwa
katika hekaheka, lakini Nadir Haroub, Andrey Coutinho na Haruna Niyonzima kwa
nyakati tofauti walishindwa kutumbukiza mpira wavuni.
Kikosi cha Yanga kilipangwa hivi: Ally Mustapha,
Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Salum Telela, Simon
Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe/Jerry Tegete, Mrisho Ngassa na
Andrey Coutinho/Kpah Sherman.
No comments:
Post a Comment