HUU NDIO UZEMBE KATIKA DENI LA ATCL, UNAKARIBIANA NA HUJUMA


Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amesema katika kuangalia deni la Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), inaonesha kuwapo uzembe unaokaribiana na hujuma.

Amesema makosa ya nyuma yaliyotokea kwenye ATCL, ni ya hovyo na ameshauri wabunge watunge sheria za kubana watu aliowaita wa hovyo waliosababisha tatizo hilo.
“Katika kuangalia deni la ATCL, ni uzembe unaokaribiana na hujuma…sina  uhakika kama wahusika wa kashfa hiyo wamepatiwa ‘dawa’ inayostahili,” alisema Sitta jana bungeni alipokuwa akijadili taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu matumizi ya mashirika ya umma.
Waziri Sitta alikuwa akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge wakati wa mjadala wa kuchangia taarifa ya kazi za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuanzia Januari 2014 hadi Januari 2015.
“Huko tuendako tutunge sheria za kubana watu wa hovyo hovyo. Ukilitazama deni la ATCL ni uzembe unaokaribiana na hujuma. Sina hakika kama wahusika wamepatiwa dawa yao. Si ajabu wanatamba tu,” alisema Sitta.
Sitta, ambaye aliupongeza uongozi wa Dk Harrison Mwakyembe katika wizara hiyo ya Uchukuzi, aliwahakikishia wabunge kwamba kama ilivyo kawaida yake ya uongozi wa viwango na kasi, watashangaa mambo yanayokuja ni makubwa.
“Kama ilivyo kawaida yangu ya kuongoza kwa viwango na kasi, mtashangaa hayo yanayokuja,” alisema. Alisisitiza kwamba, muda ulio mbele yake wa kuongoza wizara unaonekana ni mfupi, lakini si mfupi kwa sekta binafsi kwani yako mambo mengi yataanza kufanyika kwa ubia.
Alisema kabla ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake, ujenzi wa Reli ya Kati utakuwa umeanza. 
Wakati huo huo, alisema reli ya Tanga-Arusha-Musoma, wanakamilisha usanifu   kwa mtindo wa kushirikisha sekta binafsi na serikali inaamini kwamba hiyo nayo itafikia hatua ambazo kazi ya kujenga imekaribia.
Pia reli ya kutoka Mtwara hadi Mbambabay hadi tawi la kwenda Liganga na Mchuchuma, itakuwa imefikia hatua ya juu ya utekelezaji.
Kuhusu mambo yanayozonga sekta ya reli, hasa ya jijini Dar es Salaam maarufu kama ‘Treni ya Mwakyembe’, alisema  inatumia injini mbili sasa kwa sababu hakuna mahali pa kugeuza.
Hata hivyo, Waziri Sitta alisema, Jumanne atakutana na Wajerumani wanaokuja nchini katika ziara ya Rais wao, ambao wanakuja na utaalamu utakaotumika katika reli hiyo ya jijini Dar es Salaam. 
“Wakazi wa Dar es Salaam wategemee kuboreshewa na hata kuongezwa ifike Pugu,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa  PAC, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto, alisema mabilioni ya fedha yanayoendelea kulipwa kwa Kampuni ya Wallis, kwa huduma ya ndege iliyofanya kazi nchini kwa miezi sita na kisha ndege hiyo kupelekwa Ufaransa kwa matengenezo, ni fedheha kubwa kwa wazalendo wa taifa hili.
“Ndege ilikodishwa kwingine wakati bado ina mkataba na Tanzania. Lazima tushitaki hiyo kampuni kwanza. Watu waliohusika na mkataba wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema Zitto na kuongeza kwamba pendekezo hilo limekuja mara ya pili kwani walianza mwaka 2011 kuagiza juu ya suala hilo.
Kwa mujibu wa Zitto, kampuni iliyohusika katika ujenzi wa chumba cha watu maalumu katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege Mwalimu Julius Nyerere, ikidaiwa ametumia Sh bilioni 12 wakati alitumia Sh bilioni tatu, pia inahusika katika suala la ATCL.
Zitto aliomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuchunguza kampuni hiyo ya Walllis  kuhusu uendeshaji wa shughuli zake nchini. 
Taarifa ya PAC inaonesha baada ya kuvunjika kwa mkataba wa ubia baina ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na ATC, Machi 2008, Wizara ya Miundombinu wakati huo, iliingia makubaliano na Kampuni ya China Sonangol ya China, kwamba ingeleta ndege mpya saba kwa ATCL ikiwamo tano aina ya Airbus ambazo zingewasili mwaka 2012/13.
Wakati ndege zikisubiriwa, Sonangol ilitambulisha Kampuni ya Wallis Trading Inc kwa ATCL na kisha ziliingia mkataba wa ukodishaji ndege aina ya Airbus 320 kwa kipindi cha miaka sita kwa malipo ya dola za Marekani 370,000 kila mwezi.
Kwa mujibu wa Zitto, huo ulikuwa mwanzo wa mwisho wa ATCL kwani baada ya ndege hiyo kuwasili, ilifanya kazi kwa miezi sita pekee na baadaye ilifungiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCCA), kwa kushindwa kutekeleza matakwa ya usafiri wa anga.
Ndege hiyo ilipelekwa Ufaransa kwa matengenezo makubwa Julai 2009 na haijawahi kurudi ambapo Serikali kama mdhamini wa ATCL, inadaiwa fedha nyingi na Kampuni ya Wallis.
Deni la ATCL kwa Wallis kwa mujibu wa Zitto, linafikia dola za Marekani milioni 42 na kutokana na majadiliano mbalimbali, Serikali imeshalipa jumla ya dola milioni 26 hadi sasa huku baki inayodaiwa ikiwa dola milioni 23.
Taarifa zinasema ndege hiyo ikiwa Ufaransa, ilipakwa rangi na kukodishwa kwa Shirika la Ndege la Nchi ya Guinea wakati Serikali ikiendelea kulipia tozo ya ukodishaji wa ndege husika.
Kuhusu hali mbaya ya Kampuni ya Simu (TTCL), imekubaliwa Serikali imilikishe Mkongo wa Taifa kwa kampuni hiyo iuendeshe. Pia madeni ambayo Serikali inaidai kampuni hiyo, iyageuze kuwa mtaji.
Mapendekezo mengine yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa PAC, Kabwe Zitto ni eneo la misamaha ya kodi, ambalo kamati ilipendekeza Mamlaka ya Mapato (TRA) iagizwe kuanzia sasa kila mwezi, wanapotangaza makusanyo ya kodi pia watangaze misamaha iliyotolewa katika kipindi hicho.
Kuhusu madeni ya Serikali kwa mifuko ya jamii, wabunge wameridhia PAC kuibana Serikali kuhakikisha hatifungani inatolewa na Serikali kuokoa mifuko na wakati huo huo kufanya serikali kuwa na nidhamu ya kukopa.
Zitto aliwasilisha mapendekezo na maoni hayo juzi bungeni wakati akihitimisha hoja za wabunge wakati wa mjadala wa taarifa ya mwaka ya PAC kuhusu hesabu zilizokaguliwa na serikali kuu na mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni 30, 2013.
Kuhusu Mamlaka ya Bandari (TPA), Zitto alisema imeongeza ufanisi kutokana na mapato kukua kutoka Sh bilioni  320 hadi Sh bilioni  537 katika kipindi cha miaka mwili.
Hata hivyo, alisema ipo kesi yenye thamani ya Sh bilioni 330 ambayo  Serikali iliingia makubaliano na mkandarasi mwaka 1970. Alishauri Serikali kuangalia kesi hiyo vinginevyo, inaweza kugharimu fedha nyingi.

No comments: