CLOUDS MEDIA GROUP WAKANUSHA KUUZWA


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Clouds Media Group, Joseph Kusaga amesema kuwa habari zilizoenea mtaani kwamba kampuni hiyo imeuzwa ni za uzushi na kuwataka Watanzania wazipuuze.

Kampuni hiyo ambayo inamiliki Clouds FM, Clouds Tv na Choice FM ilidaiwa kuuzwa kwa mmoja wa wafanyabiashara maarufu na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kusaga (pichani) alisema habari hizo ambazo zilisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii zilisababisha usumbufu mkubwa kwa wafanyakazi na  viongozi wa Clouds  pamoja na Watanzania kwa ujumla.
Alisema habari hiyo imetengenezwa na watu walioamua kupoteza muda wao katika mitandao ya kijamii, lakini wapo wanaovuna fedha nyingi kwa kupitia njia hiyo ya mawasiliano.
Alisema mara baada ya kuenea kwa habari hiyo, usumbufu mkubwa uliibuka kutokana na watu wenye mapenzi mema na kampuni hiyo kuanza kuhoji juu ya taarifa hizo kama zina ukweli.
“Clouds Media Group ni kampuni iliyoanzia chini kwa ushirikiano wa watu wengi, hivyo kuamua kuiuza kiholela ni jambo la kushangaza, ingawa pia si dhambi kufanya hivyo kwa mtu yoyote kwa sababu ni biashara kama zilivyokuwa biashara nyinginge," alisema.
Aidha Kusaga aliwahakikishia Watanzania kuwa Clouds ni chombo huru kisichofungamana na chama chochote cha siasa, huku akisema kwamba katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu haki itatolewa kwa vyama vyote na wanasiasa wote.
“Huu ni mwaka mgumu, hivyo naomba niseme ikitokea suala la kuhoji au kuunga mkono siasa, basi haki itatolewa kwa wanasiasa wote, ukizingatia kwamba chombo chetu hakika chama cha siasa inachokiunga mkono kwa sababu zozote zile,” alisema Kusaga.

No comments: