HOSPITALI ZA MIKOA 25 KUBORESHWA


Hospitali 26 za rufaa katika mikoa 25 nchini, zitafanyiwa  maboresho ili zitoe huduma bora za afya kupitia mradi wa Japan International Co-operative Agency (JICA) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Akizungumza katika mkutano wa tathimini ya miradi mingine ya afya iliyotekelezwa,  mwakilishi wa shirika la Jica, Kuniaki Amatsu alisema mpango huo umeonesha ufanisi mkubwa katika utekelezaji wake na kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya.
“Uboreshaji wa huduma za afya umekuwa na matokeo mazuri na tumeshuhudia mabadiliko katika hospitali nyingi, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa hapo awali. Mazingira yamekuwa mazuri na utaratibu mzuri wa mpangilio wa utoaji huduma,” alisema Amatsu.
Akizungumzia hali ilivyokuwa katika hospitali nyingi za rufaa kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa uboreshaji huduma mwaka 2011, alisema kwa sasa mandhari za hospitali ni nzuri na mazingira pia yanafurahisha katika upatikanaji wa huduma za afya.
“Hospitali zimekuwa na mandhari nzuri na hata ufanisi wa utoaji huduma pia umeongezeka ikilinganisha na kipindi cha nyuma kabla mradi huu haujaanza kutekelezwa katika hospitali hizo,” alisema.
Hospitali zilizoonesha mafanikio ambazo zitaanza kutekelezewa maboresho mengine ambayo mafanikio yake yatatumika katika maboresho ya sekta ya afya Afrika ni pamoja na Mawenzi (Kilimanjaro), Bukoba (Kagera), Mbeya (Mbeya), Morogoro (Morogoro), Shinyanga (Shinyanga).
Nyingine ni Bombo (Tanga), Songea (Songea), Musoma (Mara), Maweni (Kigoma), Iringa (Iringa), Sokoine (Lindi), Amana, Mwananyamala na Temeke za Dar es Salaam, Ligua (Mtwara), Tumbi (Pwani), Sekou-Toure (Mwanza), Dodoma (Dodoma), Mount Meru (Arusha), Singida (Singida), Kitete (Tabora), Sumbawanga (Rukwa), Bariadi (Simiyu), Mpanda (Katavi), Geita (Geita), Kibena (Njombe), na Manyara (Manyara).
Akizungumzia mradi huo mpya wa uboreshaji hospitali za rufaa za mikoa utakaoanza mwezi ujao, Amatsu alisema wanahitaji kuongezea ufanisi katika utoaji wa huduma, ikiwa ni pamoja na kuwezesha watoa huduma kupata mafunzo bora ya kutoa huduma.
Watoa huduma hao pia watafundisha namna na umuhimu wa utunzaji wa kumbukumbu za kitabibu, jinsi ya kuweka mipangilio mizuri ya vifaa tiba na dawa katika mazingira ya hospitali na kutunza mazingira ya hospitali.
“Mradi mkubwa unaotarajia kuanza mwezi ujao, utajumuisha hospitali za rufaa zipatazo ishirini na sita zitakazoboreshwa kwa kupatia mafunzo madaktari na watoa huduma wengine, ili kuwa na ufanisi mzuri wa kutoa huduma za afya.
“Hospitali hizo zitapatiwa vifaa tiba kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa matibabu, kuwezesha hospitali kutatua matatizo madogo bila kuhitaji msaada wa nje na kufundisha watoa huduma jinsi ya kutunza kumbukumbu za matibabu na takwimu nyingine za kitabibu,” alisema Amatsu.
Akifungua mkutano huo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bernard Kongo, aliishukuru  Serikali ya Japan kwa kuendelea kusaidia Tanzania kuboresha huduma za afya, kwani kupitia shirika la Jica hospitali nyingi zimeboreshwa na kuwa na uwezo mkubwa wa utoaji wa huduma za afya.
Aliongeza, “mradi huu utakaoanza, utasaidia kwa kiasi kikubwa katika upanuzi wa huduma za afya hapa nchini. Hospitali zetu za rufaa zitatoa huduma za haraka na zenye ufanisi mkubwa ikilinganishwa na hapo awali,” alisema Kongo.
Akizungumzia jinsi walivyonufaika na mradi huu, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Archie Hellar, alisema hospitali za mkoa wake zimekuwa bora zaidi kwa kila kitu ukilinganisha na hapo zamani.

No comments: