AZAM YAREJEA KILELENI KWA KISHINDO, YAIVURUGA MTIBWA 5-2


Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom, Azam FC wameivurumisha Mtibwa Sugar ya Turiani kwa mabao 5-2 na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jioni hii.

Katika mechi hiyo ya kusisimua, hadi mapumziko Azam walikuwa mbele kwa mabao 3-1 yaliyowekwa kimiani na Kipre Tchetche, Frank Domayo na Didier Kavumbagu, wakati lile la Mtibwa likiwekwa kimiani na Mussa Nampaka.
Tchetche alifunga bao lake katika dakika ya 19 akiuwahi mpira Brian Majwega uliogonga mwamba na kumwacha kipa Said Mohamed akiwa hana la kufanya.
Wakati Mtibwa wakijiuliza, Domayo akaiandikia Azam bao la pili katika dakika 26 akimalizia pasi ya Majwega ndani ya sanduku la penalti.
Baada ya mabao hayo, Mtibwa ikazinduka na kufanya shambulizi lililoipatia bao la kwanza kutpitia kwa Mussa Nampaka katika dakika ya 34 akimalizia pasi ya Ally Shomari.
Kavumbagu akaingia kwenye kitabu cha wafungaji jioni ya leo baada ya kuiandikia Azam bao la tatu akimalizia pasi ya Salum Abubakar muda mfupi kabla ya mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Azam ikisukumiza mashambulizi ya nguvu langoni mwa wapinzani wao na kufanikiwa kupata bao la nne dakika ya 58 kupitia tena kwa Domayo baada ya kuuwahi mpira yliotemwa na kipa wa Mtibwa.
Mtibwa ikazinduka tena baada ya bao hilo na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 70 kupitia kwa mshambuliaji wao hatari, Ame Ally baada ya kupokea pasi kutoka kwa Abdallah Juma aliyeingia muda mfupi kuchukua nafasi ya Mussa Hassan ‘Mgosi.
Wakati kila mtu akiamini matokeo yangebaki hivyo, Tchetche akahitimisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la tano kwa Azam katika dakika ya 86 akiunganisha krosi ya Shomary Kapombe.
Kwa matokeo hayo, Azam sasa imefikisha pointi 25 sawa na Yanga, lakini wanaongoza kutokana na wastani mzuri walionao wa mabao ya kufunga na kufungwa, zote zikiwa zimecheza mechi 13.
(Picha kwa hisani ya blogu ya bongostaz).

No comments: