WAFUNIKWA NA KIFUSI WAKICHIMBA VITO TANGA


Wakazi wawili wa kata ya Kigongoi wilayani Mkinga, wamekufa papo hapo baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo walipokuwa wakichimba madini aina ya vito.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki alibainisha hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu matukio mbalimbali mkoani humo.
Aliwataja waliokufa ni Nyange Mussa (21) ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Hemsambia na Kagembe Shabani (19) wa kitongoji cha Shashui kata ya Kigongoi wilayani Mkinga.
“Ajali hii iliyosababisha vifo ilitokea juzi kwenye eneo la mgodi unaomilikiwa na Charles Kifunta wakati wahusika walipokuwa ndani ya mgodi ghafla walishukiwa na gema la udongo (kifusi) na kufa papo hapo”, alisema. 
Kamanda Ndaki (pichani) alisema katika tukio hilo, Alex Remo (24) amejeruhiwa. Hata hivyo alisema hali ya afya yake kwa sasa inaendelea vizuri. 
Alisema hakuna mtu aliyekamatwa kuhusu tukio hilo, ingawa uchunguzi wa polisi unaendelea.

No comments: