Wanafunzi 84 wa Chuo Kikuu
UDOM wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuhamasisha uvunjifu wa amani chuoni
hapo.
Wanafunzi hao walikamatwa
wakifanya maandamano kutoka chuoni hapo kuelekea katika ofisi mbalimbali za
viongozi wa Serikali zilizopo Dodoma mjini majira ya saa kumi na moja alfajiri.
Kamanda wa Polisi mkoa wa
Dodoma, David Misime alisema wahusika wa vurugu hizo ni wanafunzi wa programu maalumu
ya diploma ya ualimu.
Imeelezwa kuwa awali
wanafunzi hao juzi walifanya kikao ambapo walitoka na maazimio ya kudai
ongezeko la posho ya chakula na kupinga kucheleweshwa malipo hayo.
Pamoja na kutoka na madai
hayo yaliyofikishwa kwa uongozi, uongozi uliwaeleza kuwa wenye mamlaka ya
kuzungumzia suala la kuongezewa posho ni Bodi ya Mikopo na siyo chuo na
kuwataka kufuata taratibu kuwasilisha madai yao.
Hata hivyo, walielezwa kuwa
hundi kwa ajili ya fedha za posho zao zimeshasainiwa na kuwasilishwa benki ili
waweze kuanza kupewa posho zao, lakini hawakuridhika.
“Hata hivyo, wanafunzi hao
hawakuridhika na usiku wakaanza kuhamasishana kufanya maandamano jambo ambalo
ni kosa kisheria,” alisema Kamanda Misime.
Aliongeza kuwa, wanafunzi hao
wamehojiwa kulingana na ushahidi ambao umekusanywa na wamefikishwa mahakamani
kwa kosa la kufanya maandamano yasiyo na kibali.
Aidha, alisema viongozi
waliohamasisha uvunjifu huo wa sheria baadhi yao wamekamatwa na baadhi
wanaendelea kutafutwa ili nao waweze kuchukuliwa hatua stahiki.
Ushahidi uliokusanywa
unaonesha jinsi viongozi hao wameshiriki kuhamasisha kupitia vikao rasmi na
visivyo rasmi, katika vikundi, kupita katika mabweni na kutuma ujumbe mfupi wa
simu (SMS).
Kamanda huyo wa Polisi alitoa
wito kwa wanafunzi hao kutumia taratibu zilizowekwa na Serikali na Chuo
kuwasilisha malalamiko yao ngazi kwa ngazi na siyo kufanya vitendo vya kuvunja
sheria ambavyo vitawasababishia kupambana na vyombo vya dola.
Wanafunzi hao ambao ni wa
programu maalumu kwa ajili ya walimu wa masomo ya Hesabu, Fizikia, Kemia,
Baiolojia na Tehama yenye wanafunzi zaidi ya 3,000 wanasema wataendelea na
maandamano na mgomo wakitaka kumuona Rais au Waziri Mkuu ambao ndio wamekuwa
wakihimiza programu hiyo maalumu.
Mmoja wa wanafunzi hao, Yuda
Mases akizungumza na gazeti hili alisema maandamano yao yaliyokuwa ya amani
yalikumbana na vikwazo vya polisi ambavyo vilifanya waingie mjini kwa mtindo wa
makundi.
Alisema wenzao wapatao 100
akiwemo Rais na Waziri Mkuu wa Serikali ya Udom programu maalumu wametiwa mbaroni
katika juhudi za wazi za wanafunzi hao kutaka serikali iwaangalie kutokana na
kukosa fedha za chakula ambazo zimechukuliwa na Chuo Kikuu cha UDOM.
“Tangu Novemba 8, mwaka jana
tumefika hapa tumelipwa Sh 367,500 kama hela ya chakula kwa siku 60 kamili,
lakini fedha hizo zilikatwa na UDOM Sh 282,500 kama Direct Cost na hii imeleta
shida kwa wanafunzi,” alisema Moses ambaye amedai kuwa kwa sasa kila siku mbili
watu wanaanguka kwa kukosa chakula.
Alisema maandamano yao ni
kutaka kuwaambia viongozi waliosimamia programu hiyo maalumu Rais Jakaya
Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda waone haki inatendeka kuhusu fedha,
malazi, vitabu na vitamkwa (vilivyoorodheshwa katika barua za kuwaita).
Alisema kwamba programu hiyo
ina watu takribani 3,000 wakiwa wametawanyika katika vitivo vitatu vya Tehama,
Elimu na Sayansi Jamii.
Makamu Mkuu wa chuo hicho,
Profesa Idrisa Kikula hakupatikana kuzungumzia suala hilo, kwani alipotafutwa
ilielezwa yupo kwenye kikao.
No comments:
Post a Comment