WAKILI MWALE NA WENZAKE WASOMEWA MASHITAKA MAPYA 42


Mwanasheria na wakili maarufu wa kujitegemea wa jijini hapa,  Medium Mwale anayemiliki kampuni ya uwakili ya JJ Mwale Advocates na wenzake watatu jana walisomewa mashitaka mapya 42  ya utakatishaji fedha haramu, kula njama na kughushi baadhi ya nyaraka na kujipatia kiasi cha Sh bilioni 18.

Mbali ya Mwale wengine walioshitakiwa na mwanasheria huyo ni pamoja na Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Mapato jijini Arusha, Boniface Thomas mwingine ni mfanyabiashara wa jijini Nairobi DonBosco Gichana, Bob James Onderi na Elias Ndejembi.
Awali katika kesi ya msingi iliyosomwa Agosti,  2011, Mwale na wenzake walisomewa mashitaka 30 na wakili mwandamizi wa Serikali Frederick Manyanda na ilidaiwa kuwa mtuhumiwa huyo na wenzake wanatuhumiwa kujipatia zaidi ya Sh 18 kwa njia haramu ya utakatishaji fedha haramu ikiwa ni pamoja na kughushi nyaraka na kuhujumu uchumi.
Akiwasomea mashitaka Mwendesha mashitaka wa serikali Tiba Byekomya na mwenzake Felix Kwetukia walidai mbele ya Hakimu Mfawidhi Mustapher Sinayi kuwa ushahidi wa kesi hiyo umekamilika na wanatarajia kupeleka mashahidi 41 katika kesi .
Hakimu Mfawidhi Siyani aliwaeleza watuhumiwa kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwani Mahakama yenye haki ya kisheria kusikiliza kesi hiyo ni Mahakama Kuu Kanda ya Arusha. 
Baada ya maelezo hayo Mwanasheria wa Serikali aliwasilisha majina ya mashahidi 41 ambao watakwenda Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kutoa ushahidi wa kesi hiyo.
 Kuanza kwa usikilizwaji wa kesi hiyo kumewezeshwa na kukamilishwa kwa upelelezi uliodumu kwa zaidi ya miaka minne sasa.

No comments: