SIMBACHAWENE, MWIJAGE WAAHIDI KASI KATIKA UMEME


Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene na Naibu wake, Charles Mwijage waliripoti katika ofisi zao mpya na kuahidi kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na kuhakikisha wanasambaza umeme vijijini kwa kasi.

Aidha, wamesema vipaumbele vyao katika kutumikia wananchi ni umeme, mafuta, madini na gesi.
Simbachawene alisema uongozi wake utahakikisha umeme unasambazwa vijijini kwa kasi ile ile kwa kushirikiana na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
“ Tutahakikisha kasi ile ile ya kupeleka umeme vijijini iliyofanywa na waliopita, tutaenda nao ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme huku tukikimbizana na muda uliobaki.
Kwa upande wa mafuta, Simbachawene alisema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), watahakikisha bei ya mafuta inapungua kulingana na bei ya soko la kimataifa ili kuhakikisha watanzania wanapata bidhaa hiyo kwa bei nafuu zaidi.
Alisema upande wa sekta ya madini, wanatambua changamoto ya matabaka ya wachimbaji wadogo, kati na wakubwa na kuwa kazi yao kubwa itakuwa ni kuhakikisha kila tabaka haliumizi tabaka jingine na kujenga fursa kwa wachimbaji wadogo kwa mujibu wa sheria na sera ya madini.
Kuhusu sekta ya gesi, alisema sekta hiyo ambayo inaiingiza nchi katika biashara ya kimataifa, watahakikisha inasaidia wazawa na pia kupunguza gharama za maisha kutokana na kupungua kwa bei ya umeme baada ya kuanza kutumika katika kuzalisha umeme.
Alipoulizwa kuhusu mzozo uliopo wa kuwapo kwa usiri wa mikataba ya mafuta na gesi, Simbachawene alisema anachojua kuwa mikataba hiyo iko wazi na wabunge wana uwezo wa kuiona, lakini aliomba muda wa kuliangalia suala hilo.
“ Ninavyojua mikataba iko wazi, wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi wana uwezo wa kuiona, sasa huo uwazi sijui ni kwenda kuibandika soko la Kariakoo? Lakini nipeni muda kuangalia hili na tutalitolea maelezo hapo baadaye,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu kutiliwa shaka uwezo wake na baadhi ya wanasiasa, Simbachawene alisema ana uwezo wa kuongoza wizara hiyo na kuwa hawezi kuzuia watu wengine kuwa na wa mawazo ya kumtilia shaka.
“ Nimekuwa mbunge wa kuchaguliwa kwa miaka 10, baada ya kuchaguliwa vipindi viwili, pia nimekuwa naibu waziri wa wizara hii na rekodi zangu zinafahamika.
“ Lakini sio ajabu kama mtu anakutilia shaka, Yesu mwenyewe kuna watu walimuamini na wengine walimtilia shaka mpaka leo. Nina shahada mbili nimezipata hapa hapa nchini, bado natiliwa shaka, tukiacha vyeti kila mtu Mungu anampa karama, hivyo acheni Mungu afanye kazi yake.”
Naye Naibu wake, Mwijage alisema kuwa kazi aliyotumwa na Rais Kikwete ni kumsaidia waziri katika sekta ya nishati huku akisema anafahamu changamoto zinazoikabili wizara hiyo, ikiwamo kilio cha wachimbaji wadogo wa madini.

No comments: