MUHIMBILI KUWEKA HISTORIA YA TIBA YA MOYO AFRIKA MASHARIKI


Wakati ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) na hospitali ya kutoa huduma na kufundishia kwa vitendo katika kijiji cha Mloganzila huko Kibamba ukiendelea, chuo hicho kinatarajia kujenga kituo cha tiba ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu cha kwanza Afrika Mashariki.

Kituo hicho kinachoelezwa kitakuwa ni cha kwanza kwa Afrika Mashariki, kitakuwa kikitoa mafunzo na tiba kwa wananchi wa nchi hizo za Afrika Mashariki.
Hayo yameelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Ephata Kaaya, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alipotembelea eneo hilo, kuangalia maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho.
Alisema tayari wameshasaini mkataba na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya kwanza ya kituo hicho, ambapo awamu ya kwanza inayotarajiwa kuanza wakati wowote itakuwa ni kwa ajili ya kituo cha mafunzo cha magonjwa hayo, huku vituo vingine vitakuwa katika nchi za Kenya, Uganda na Rwanda.
“Awamu ya kwanza itajumuisha ujenzi wa madarasa, maabara, vyumba vya utafiti pamoja na vitu vyote kwa ajili ya kujifunza ili awamu ya pili itakapokuja itakayokuwa ni ujenzi wa hospitali tayari tutakuwa na madaktari bingwa,” alisema Profesa Kaaya.
Alisema benki hiyo imetoa dola za Marekani milioni 9.75 (Sh bilioni 16.5) huku serikali itaongezea kiasi kingine cha fedha kwa ajili ya ujenzi huo kuanza.
Akizungumzia ujenzi wa chuo kipya pamoja na hospitali ya kisasa, Profesa Kaaya alisema ujenzi huo utakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 15,000.
Waziri Kawambwa alisema ili mji huo wa tiba wa Mloganzila uweze kukamilika ni lazima kuwapo na chuo kitakachoenda sambamba na hospitali hiyo ili kiwe na wataalamu wengi na wa uhakika.
Alisema katika bajeti ijayo ni lazima serikali itenge fedha kwa ajili ya chuo hicho, kampasi ya Mloganzila. Alisema kwa sasa changamoto ya tiba iko katika sehemu nzuri hivyo jitihada ziongezwe ili ifike mahali Watanzania waondokane na gharama za kwenda nje ya nchi kufuata matibabu.

No comments: