MELI YAZAMA NA KUUA WATU 14, BASI LAPINDUKA NA KUUA WANNE

Watu 18 wamepoteza maisha katika ajali mbili tofauti, ambapo katika ajali ya majini meli iliyobeba shehena ya mahindi imezama na kuua watu 14, wakati katika ajali ya barabarani, basi kutoka Handeni mkoani Tanga kwenda Dar es Salaam limeua watu wanne.
 
Katika ajali ya majini, Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda  alisema abiria 14 kutoka nchi jirani ya Burundi wanahofiwa kufa maji baada ya meli ya mizigo waliyokuwa wakisafiria, kuzama eneo la kijiji cha Kala mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi mkoani Rukwa.
Kamanda alisema meli hiyo ni Mv Mbaza na ilisajiliwa Burundi. Ilikuwa na shehena ya mahindi tani 437 na watu 15.
Alisema meli hiyo iliondoka katika bandari ya Kasanga wilayani Kalambo mkoani Rukwa Januari 10 mwaka huu kati ya saa 5 na 6 usiku na saa mbili baadaye ilizama eneo la kijiji cha Kala.
"Taarifa zilizopo ambazo zimethibitishwa na wamiliki wa meli hiyo waliopo Burundi ni kwamba wafanyakazi 13 kati ya 14 wa meli hiyo na abiria mmoja wanahofiwa kufa maji," alieleza.
Kamanda  alisema ni mfanyakazi mmoja pekee ndiye aliyeokolewa na meli nyingine ya Burundi iitwayo Mv Teza, iliyokuwa ikitokea bandari ya Mpulungu nchini Zambia ikielekea nchini Burundi.
"Mtu huyo aliokolewa Januari 13, mwaka huu ambapo hadi sasa bado hajapata fahamu...hivyo kushindwa kupata taarifa za chanzo cha ajali hiyo," alisema.
Kamanda Mwaruanda alisema hadi sasa hakuna mwili wowote ule ulioopolewa wala kuonekana. Alisema hapakuwepo na mawasiliano ya redio kati ya bandari na meli hiyo, kwani bandari  hiyo ya Kasanga haina mawasiliano yoyote, zaidi ya simu za mkononi.
"Maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika vikiwemo vijiji vya Kala, Wampembe na Mpasa wilayani Nkasi hakuna mawasiliano yoyote yale ya simu. Meli hiyo iliruhusiwa kuondoka usiku katika bandari ndogo ikiwa haina vifaa vyovyote vya mawasiliano,” alisema.
Ofisa Mamlaka ya Uthibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) mkoa wa Rukwa, David Charagi alieleza kuwa meli hiyo ilifuata taratibu zote za ukaguzi katika forodha ya Kasanga na kuruhusiwa kuendelea na safari.
Kutoka Kibaha inaripotiwa kuwa, watu wanne wamekufa baada ya basi kampuni ya Hajees, walilokuwa wakisafiria kutoka Handeni kwenda Tanga kuacha njia na kupinduka.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 2:00 katika kijiji cha Mnazi, kata ya Mandela wilayani Bagamoyo na ilihusisha basi hilo, aina ya Scania lenye namba za usajili T 834 BAU. Alisema basi hilo lilipinduka na watu hao wanne walikufa papo hapo.
Alitaja waliokufa ni kondakta wa basi hilo, Mkomwa Juma (35) mkazi wa Kimange, Siasa Iddi (25) mkazi wa Kwamakocho, Mayunga Ramadhan (45) na Rehema Omar 35.
Miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo.

No comments: