BEI ZA PETROLI NA DIZELI KUSHUKA ZAIDI MACHI

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imebainisha kuwa hadi kufikia Machi mwaka huu, bei ya mafuta nchini itaendelea kushuka kulingana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Hata hivyo, mamlaka hiyo imeonya kuwa bei hiyo ya mafuta nchini haitaweza kupungua kwa kiasi kikubwa, kutokana na kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya dola ya Marekani pamoja na kutokubadilika kwa ushuru mbalimbali wa ndani wa mafuta.
Pamoja na hayo, Kampuni ya Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PICL) imeiomba Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini kuingilia kati na kuihamasisha Serikali iongeze ulinzi katika mabomba na matangi ya mafuta Kurasini, ambayo kwa sasa hayako salama na ni hatari kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Akiwasilisha taarifa ya ukokotoaji wa mafuta kwa kamati hiyo Dar es Salaam jana, Mtaalamu kutoka EWURA, Lorivii Long’idu, alikiri kuwa ni kweli kwa sasa bei ya mafuta katika soko la dunia imekuwa ikishuka kwa kasi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
“Bei hizi zimeshuka kutoka dola 100 hadi kufikia dola 60 kwa pipa ambayo ni sawa na asilimia 40 kutokana na kudorora kwa uchumi wa bara la Ulaya katika kipindi hiki na kuwepo kwa tofauti za mitazamo ya kisiasa hasa katika nchi za Marekani na Urusi,” alisema Long’idu.
Hata hivyo, alisema pamoja na bei hizo kushuka tangu Julai hadi Desemba mwaka jana, kwa kawaida kwa Tanzania huchukua takribani miezi miwili bei hiyo kuweza kufikia soko la ndani.
Alisema bei zote za mafuta katika soko la ndani, zimekuwa zikishuka kuanzia robo ya mwisho wa mwaka jana sambamba na kushuka katika soko la dunia na kwamba bei hizo hukokotolewa na Ewura kwa kutumia kanuni maalum, inayotumia gharama halisi za uagizaji mafuta nchini, zinazotokana na meli za mafuta yaliyopokelewa mwezi husika yaliyonunuliwa mwezi wa nyuma yake.
Alisema uhusiano wa bei za soko la dunia na soko la ndani, unapishana kwa miezi miwili na kwamba mafuta yanayotumika mwezi huu, Ewura ilikokotoa bei zake tangu Novemba kulingana na bei ya mafuta yaliyonunuliwa katika soko la dunia mwezi huo.
Long’idu alisema kwa hali ilivyo sasa bei za mafuta ghafi katika soko la dunia, zitaendelea kushuka kama hakutakuwa na tukio lisilo la kawaida duniani, hali itakayochangia kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo katika soko la ndani japo si kwa kiwango sawia.
Alisema pamoja na bei kushuka katika soko la dunia kwa kiwango chochote kile, bei ya ndani itashuka kulingana na thamani ya Shilingi dhidi ya dola ya Marekani lakini pia ushuru uliopo ambao katika petroli unatozwa Sh 878, dizeli Sh 754 na mafuta ya taa Sh 701 kwa lita ambao wenyewe haubadiliki.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Nishati na Madini, Jerome Bwanausi, aliagiza Ewura na PICL wanapokokotoa bei za mafuta kuhakikisha wanatoa ufafanuzi wa hali halisi ya bei za soko la dunia na utaratibu mzima wa uingizaji wa mafuta nchini ili kuondoa habari potofu zinazosambazwa juu ya bei hizo za mafuta.
Aidha, aliagiza Wizara ya Nishati na Madini kuchukua hatua za haraka na kushughulikia suala la ulinzi katika mabomba na matangi ya mafuta ili kudhibiti hali ya hatari ya kulipuliwa kwa matangi hayo na kuhatarisha usalama wa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
“Hii ni hatari sana kwa namna yale mabomba yalivyo hayana ulinzi, watu wanatoboa mabomba na kuiba mafuta na kuweka maboya, endapo mtu yeyote akitupa moto pale Dar es Salaam nzima itakuwa haipo, hatua za haraka zichukuliwe, na kamati ipatiwe taarifa za ulinzi wa sasa katika eneo hilo,” alisisitiza.
Aidha, alisema kutokana na hali ya hatari ya usafirishaji wa mafuta iliyopo sasa kupitia malori hasa katika vijiji malori hayo yanakopita na kulala, ni vyema Serikali ikaanza mchakato wa kuchimba mabomba ya kusafirishia mafuta na kufufua reli ili kudhibiti usalama wa wananchi.

No comments: