Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amewataka Watanzania kutoa
taarifa kuhusu makusudio ya kuuza nyumba za Serikali na mashirika ya umma,
kutokana na madeni mbalimbali ili ziweze kukombolewa kabla ya kuuzwa.
Akizungumza Ikulu Dar es Salaam juzi,
Balozi Sefue alisema kumejitokeza mtindo wa kukamata nyumba za Serikali na
mashirika ya umma na kuzipiga mnada, kutokana na madeni yanayodaiwa kwa
Serikali au mashirika hayo.
“Sisi tumeona hii si sawa, unakuta
nyumba ya Serikali inaweza kuwa na thamani labda ya Sh bilioni moja inauzwa kwa
Sh milioni 100…mkiona nyumba ya Serikali inauzwa, toeni taarifa tuikomboe,” alisema.
Alisema baada ya kuikomboa, watendaji
husika walioachia nyumba ya Serikali ikataka kupigwa mnada, watashughulikiwa
kwa uzembe baada ya kukomboa nyumba husika.
Balozi Sefue pia aliwataka Watanzania
kuepuka kununua nyumba za umma, kwa kuwa hata baada ya ununuzi, Serikali
haitakubali, bali itatafuta namna ya
kukomboa nyumba yake.
Hata hivyo, alikiri ugumu wa kukomboa
nyumba kama imeshauzwa kisheria, kwamba ni pamoja na kufungua kesi ya kuomba
kurejeshewa, utaratibu aliosema ni wa kisheria na mgumu.
Kutokana na ugumu huo, alisema ndiyo
maana wanaomba Watanzania kutoa taarifa mapema kabla hazijapigwa mnada ili
Serikali izikomboe.
Akitoa mfano, alisema Serikali iko
katika mkakati wa kukomboa jengo la Shirika la Ndege (ATCL) lililopo katikati
ya Jiji la Dar es Salaam, ambalo linatakiwa kupigwa mnada kulipa deni la
shirika hilo.
Katika hatua nyingine, Balozi Sefue
alisisitiza Watanzania kuepuka kutumiwa na matapeli wanaotumia jina la Ikulu.
Alisema matapeli hao, ambao Mkurugenzi
wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu ameshaongelea, wanapaswa kuepukwa.
Alitoa mfano wa watu ambao huletwa
mpaka katika geti la Ikulu na mwenyeji kuingia ndani, kisha anazubaa kwa muda
na kutoka na kutaka alipwe fedha kwa
madai ameshafanya kazi aliyotumwa Ikulu, ikiwemo ya kutafutiwa kazi.
No comments:
Post a Comment