EAC WATUMBUA BILIONI 6/- KUNUNUA TIKETI ZA NDEGE


Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo bajeti yake ya uendeshaji inategemea kwa kiasi kikubwa fedha kutoka kwa nchi wahisani, imeingia kwenye kashfa ya kupoteza mabilioni ya fedha wanayojilipa maofisa wake kutokana na safari za nje ya ofisi.

Asilimia 60 ya bajeti ya EAC inategemea michango ya wahisani, lakini Kamati ya Hesabu ya Bunge la Afrika Mashariki jana iliweka hadharani namna maofisa waandamizi wa jumuiya hiyo wanavyotumbua maisha, huku kiasi kikubwa kikitumika kununua tiketi za ndege.
 Kamati  hiyo kwenye ripoti yake imebaini kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa katika manunuzi ya tiketi za ndege ndani ya jumuiya hiyo, yenye makao yake makuu mjini Arusha, ambako Sh bilioni 6 peke yake zimetumika kuwasafirisha kwa ndege.
Pia, imebainika kuwa maofisa wa jumuiya hiyo wametumia fedha nyingi kulipa posho za kusafiria, ikiwemo posho ya kujikimu, ambazo wamejilipa, wengi wao wakiwa ni maofisa waandamizi ambao posho yao iko juu.
 Kwa upande wa Mahakama ya Afrika Mashariki, kamati hiyo imebaini  kuwepo madudu kutokana na kikao kimoja ambacho kilifanyika nje ya ofisi kupitia mpango mkakati, ambapo maofisa wake walijilipa Sh milioni 205 ambazo ni nje ya posho za kawaida za kila siku wanazostahili kupewa.
 Licha ya kuwa shughuli wanazofanya ni za kawaida, ripoti ya kamati ya Bunge imeeleza kuwa fedha nyingi za jumuiya hiyo, zisingetumika iwapo shughuli na vikao vya jumuiya hiyo vingefanyika ofisini kwake.
 Kamati hiyo ya Bunge la EALA imefafanua kwenye ripoti yake kuwa imegundua kuwepo kwa malipo yasiyo ya kawaida ya zaidi ya Sh  milioni 16, ambazo zimelipwa kwa maofisa wa jumuiya hiyo kama posho ya kujikimu, kutokana na kuhudhuria kamati ya mazishi.
Kutokana na hali hiyo, kamati hiyo imeshauri kuwa baraza la mawaziri wa jumuiya hiyo ni vyema wakaweka mwongozo kwa vifo ambavyo vitaifanya jumuiya hiyo pamoja na taasisi zake kugharimia.
 Katika matumizi ya fedha nyingi kutumika kwenye safari za maofisa hao, kamati hiyo imeielekeza sekretarieti ya jumuiya hiyo  kuweka ukomo wa siku ambazo ofisa wa jumuiya hiyo anaweza kuwa nje ya kituo cha kazi kwa shughuli za kiofisi.
Kamati hiyo ya Bunge ambayo imekuwa inakutana kwa wiki mbili mjini hapa, ilikuwa inachunguza namna uendeshaji  na matumizi ya fedha jumuiya hiyo, yanavyozingatia sheria na kanuni za kifedha, ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya matumizi ambayo sio ya msingi.
Wakati huo huo, kamati hiyo ya masuala ya hesabu imependekeza kwa baraza la mawaziri wa jumuiya hiyo, kushughulikia haraka changamoto mbalimbali zinazoikabili jumuiya hiyo pamoja na taasisi zake.
 Kamati hiyo ilikuwa inapitia taarifa za fedha za EAC zilizoishia Juni 30, 2013. Ripoti ya kamati hiyo inatarajiwa kujadiliwa wiki hii baada ya kuwasilishwa bungeni hapo na Mwenyekiti wa kamati ya Fedha,   Jeremie Ngendakumana.
 Kwa upande wa taarifa za fedha zinazohusu taasisi za EAC, ripoti hiyo pia ilibaini kuwepo kwa matumizi makubwa zaidi ya bajeti na hivyo wametaka baraza la mawaziri la jumuiya kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni za fedha.

No comments: