HATIMAYE MWENYEKITI WA WAFANYABIASHARA AACHIWA


Siku moja baada ya kuachiwa kwa dhamana, kutokana na kesi inayomkabili ya kudaiwa kuwachochea wafanyabiashara wasilipe kodi ya Serikali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini, Johnson Minja (34), amewataka wafanyabiashara kufungua maduka yao na kuendelea na biashara.

Pia, amewataka kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuhakikisha wanatimiza wajibu wao.
Alitoa kauli hiyo  juzi wakati akiachiwa kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Mjini. Alisema yeye hataki kuzungumzia tuhuma zinazomkabili kwa kuwa zipo mahakamani.
Hata hivyo, alisema kwamba yeye hajawahi kuchochea wafanyabiashara kuacha kulipa kodi na mara zote amekuwa akiwahimiza kulipa kodi, kwani ni wajibu wao.
 “Mimi ninao utetezi…na serikali inao ushahidi ukweli utajulikana mahakamani.. siwezi kuongelea hayo,” alisema alipokuwa akijibu hoja za waandishi.
Lakini, alisema ni vyema wafanyabiashara wasitishe mgomo na kutoa ushirikiano kwa serikali wakati mazungumzo ya kawaida kati ya wafanyabiashara na serikali kuhusu matatizo yanayokwamisha ulipaji kodi yakiendelea.
Aidha, aliitaka TRA kushirikiana na wafanyabiashara ili kuondoa vikwazo, vinavyokwamisha ulipaji kodi wenye tija kwa serikali na kwa wafanyabiashara.
Juzi wafanyabiashara wengi katika mikoa mbalimbali nchini ikiwamo Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Iringa na Dodoma walifunga maduka wakitaka kujua hatima ya Mwenyekiti wao, huku wakilalamikia mashine za kodi za kielektroniki.
Katika kesi iliyopo mbele ya Hakimu Mkazi Rebecca Minja, mtu huyo anadaiwa kuwa Septemba 6, mwaka jana katika Chuo cha Mipango Dodoma, akiwa kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania aliwashawishi Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Dodoma wasilipe kodi.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Septemba 6, mwaka jana katika Chuo Cha Mipango mshtakiwa aliwapa maelekezo wafanyabiashara wa Dodoma, wasitumie mashine za kodi za kielektroniki (EFD) za Mamlaka  ya Mapato Tanzania (TRA), ambazo zilitengenewa kwa ajili ya kuwezesha kukusanywa kwa kodi.
Mshitakiwa alikana mashtaka hayo. Alisomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali, Godfrey Wambali.
Na katika hatua nyingine, wenye maduka mkoani hapa wameyafungua, ingawa walisema kwamba bado hawapendezwi na mashine hizo, ambazo hazijali mtu akirudisha kifaa kilichonunuliwa.
Walisema mashine hizo, zina matatizo mengi yanayotia hasara wafanyabiashara na kwamba serikali inastahili kuwasikiliza na wao pia.
Wakati huo huo, Frank Leonard kutoka Iringa anaeleza kuwa wafanyabiashara  wa maduka wa wilaya za mkoa wa Iringa, wameitaka serikali kusikiliza na kuyafanyia kazi madai yao ili kuondokana na mivutano ya mara kwa mara inayodhoofisha huduma kwa wananchi.
Juzi asubuhi walifunga maduka yao, wakilenga kuvishinikiza vyombo vya dola kumuachia Mwenyekiti wao wa Taifa, Johnson Minja aliyekamatwa Dar na kisha kupandishwa kortini Dodoma.
Lakini, baada ya  Minja kuachiwa huru, baadaye juzi jioni, wafanyabiashara hao walitoa tangazo kwa wenzao wote kuendelea na biashara zao kama kawaida.
Akihojiwa, Katibu wa wafanyabiashara hao wa mkoa wa Iringa, Jackson Kalole alisema tuhuma zinazotolewa dhidi ya mwenyekiti wao wa taifa ni za uzushi.
“Minja ni mtu anayewahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi na ndio maana katika maeneo mbalimbali nchini zipo taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania kuvuka malengo yake ya kila mwaka,” alisema.
Alisema pamoja na kulipa kodi, wafanyabiashara wanayo malalamiko yao, yanayotaka mfumo wa ulipaji kodi ubadilishwe.
 “Tunataka kodi ilipwe kwenye faida, isikatwe kutoka kwenye mtaji na hilo ndio moja ya malalamiko yetu makubwa. Lakini tunataka pia kodi zote zinazoanzishwa na serikali, halmashauri zisianze kutoza kabla ya kupata maoni kutoka kwa wadau,” alisema.
Alisema wafanyabiashara wamekuwa wakigoma mara kwa mara kwa sababu serikali imeacha mianya mikubwa, inayowapotezea mapato na kufukuzana na wafanyabiashara ndogo.
 “Tumewahi kusema na tunarudia kusema pale bandarini kuna ukwepaji mkubwa wa kodi. Serikali izibe mianya hiyo na ikifanikiwa haitakuwa na sababu tena ya kufukuzana na wafanyabiashara wadogo,” alisema.

No comments: