Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
inachunguza tukio la kupigwa kwa
viongozi na wafuasi wa Chama cha
Wananchi (CUF) katika tukio la jijini Dar es Salaam juzi, kubaini kama kulikuwa
na matumizi ya nguvu ya ziada ya polisi dhidi ya raia.
Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe ambaye alisema pia ameagiza Idara ya Malalamiko
ndani ya Wizara kufanya uchunguzi kuhusu matumizi ya nguvu za ziada,
zichukuliwe hatua kwa watakaobainika kuhusika.
Waziri alikuwa akitoa taarifa bungeni, kabla
ya wabunge kujadili hoja iliyowasilishwa juzi na Mbunge wa Kuteuliwa, James
Mbatia akitaka ijadiliwe kuhusu kupigwa kwa wanachama wa CUF na matumizi ya
nguvu ya ziada yaliyofanywa na polisi katika tukio hilo la wilayani Temeke, Dar es Salaam.
“Malalamiko haya ni mazito, na Serikali
haiwezi kufumbia macho… pamoja na uchunguzi unaofanywa na Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, nimeagiza Idara ya Malalamiko ndani ya Wizara ifanye
uchunguzi kuhusu matumizi ya nguvu za ziada na ikithibitika kwamba kuna polisi
walitumia nguvu nyingi zaidi dhidi ya raia, basi tutachukua hatua mwafaka dhidi
ya wahusika wote. Na hii ni ahadi,” alisema Chikawe.
Alisema Jeshi la Polisi halipaswi kutumia
nguvu kuliko zinazohitajika katika
kukamata wahalifu wa makosa ya jinai.
“Serikali inaomba radhi kwa wananchi wote
waliokumbana na kadhia hii bila wao kujihusisha na kuwasihi wananchi kujiweka
mbali na matukio yote ya uvunjifu wa sheria,” alisisitiza.
Alisema Serikali inaendelea kuahidi kuliongoza jeshi kwa
kuzingatia sheria na maudhui yake sanjari na kukabili changamoto kuhakikisha
kunakuwa na usalama na utulivu nchi nzima.
Hata hivyo, alisema Polisi haitaogopa wala
kumwonea haya mtu yeyote bali itaendelea kutekeleza wajibu kwa kuzingatia haki
za binadamu.
Waziri Chikawe alieleza Bunge sababu za chama
hicho cha siasa kuzuiwa kufanya maandamano na kusema ni baada ya Jeshi la
Polisi kuona kwamba yanaweza kusababisha kuvunjika amani na kuathiri usalama wa
taifa.
Kwa mujibu wa Waziri, Januari 26 mwaka huu
Jeshi lilipokea barua kutoka CUF, ikitoa taarifa kuhusu kufanyika maandamano na
mkutano wa hadhara Januari 27 kuadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya wafuasi wao
yaliyotokea mwaka 2001.
Alisema baada ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam kupokea barua, iliwaita viongozi wa CUF kwa mazungumzo na
kuwafahamisha matatizo yanayoweza kutokea.
Chikawe alisema matukio ya ugaidi hususani
ulipuaji mabomu katika mikusanyiko kuwa ni miongoni mwa mambo ambayo yalihofiwa
kwamba yanaweza kutokea kupitia maandamano hayo.
Alisema Polisi baada ya kupokea barua ya CUF,
ilikutana na viongozi wao, ikawaeleza
kwamba kufanya maandamano hayo yanayolenga kuadhimisha mauaji, pia
kunaweza kusababisha chuki. Pia ilielezwa kwamba taarifa za polisi zilionesha
kunaweza kufanyika vurugu.
Waziri Chikawe alieleza Bunge kwamba, kesho
yake Polisi ilipata taarifa kuhusu kuwapo kwa mkusanyiko mkubwa wa watu kwenye
ofisi za CUF wilaya ya Temeke.
Alisema Kaimu Kamanda, Sebastian Zakaria
alikwenda na kukuta wanachama wapatao 200 wakiwa na mabango yenye maandishi
mbalimbali ikiwemo, ‘Polisi na wanajeshi acheni kutumika na CCM,’;
‘tunaadhimisha kumbukumbu ya kuuawa kwa wenzetu, polisi acheni kutunyanyasa na
kutumikia CCM kama vibaraka.’
Alisema Profesa Lipumba aliwasili katika ofisi
hizo na alionekana kukaidi zuio na kuhamasisha wanachama kufanya maandamano
kuelekea Mbagala Zakhem.
Kaimu Kamanda huyo baada ya kuona yakiendelea kinyume na zuio, alitangaza ilani
ya kutawanyika, lakini waandamanaji walikaidi.
“Ndipo akaamuru waandamanaji wakamatwe. Polisi
wakatumia mabomu,” alisema Waziri.
Waziri alisisitiza kwamba polisi wanayo
mamlaka kuzuia mkutano au maandamano, wakiridhika kwamba yanaweza kusababisha
uvunjifu wa amani.
Alisema sheria inaruhusu mtu asiyeridhika na
masharti na amri iliyotolewa, kukata rufaa kwa waziri, jambo ambalo viongozi wa
CUF hawakufanya.
Alisisitiza kwamba kilichotokea ni uvunjaji wa sheria kwa makusudi na
kutafuta umaarufu wa kisiasa.
Alisema hivi karibuni, umeibuka utamaduni mbaya
wa uvunjaji sheria. Alisisitiza kwamba haiwezekani watu waamue kwa makusudi
kutotii maelekezo ya vyombo vya usalama.
Alihimiza viongozi bila kujali vyama, itikadi
za kidini, ni wajibu wao kutii sheria za nchi na vyama vya siasa vitii sheria
bila shuruti. Alisema vurugu zinapotokea hazibagui wa kumgusa kwa maana ya
watoto, wazee na wagonjwa. “Na hii hutokea na si kwa makusudi,” alisema.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George
Masaju aligonga mwamba bungeni kuzuia mjadala huo kuhusu vurugu baada ya ushauri
wake kutozingatiwa na badala yake, Spika Anne Makinda kuuruhusu.
Baada ya Waziri Chikawe kuwasilisha taarifa
yake, Masaju alishauri Bunge lisijadili suala hilo kwa kuwa liko mahakamani.
“Jana (juzi) wakati kiti kikifanya maamuzi
kutolijadili jana isipokuwa leo (jana), Lipumba alikuwa hajafikishwa
mahakamani. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali kupitia kwa Waziri, Profesa
Lipumba alifikishwa mahakamani na akafunguliwa shauri la jinai,” alisema
Masaju.
Alisema kwa kuwa Bunge linaongozwa kwa mujibu
wa Katiba, sheria na kanuni, haliwezi kujadili jambo linalosubiri uamuzi wa Mahakama. Alisema Mahakama ni
chombo cha mwisho cha utoaji haki na wakati huo huo mihimili mitatu inapaswa
ifanye kazi bila kuingiliana majukumu yake.
“Katika mazingira kama haya, ningeshauri Bunge
lako tukufu lisilijadili suala hili,” alisema Masaju ambaye wabunge wa upinzani
waliingilia kati na kuanza kurusha maneno ya kumpinga, jambo lililozua kelele
bungeni.
Mwanasheria huyo wa Serikali alilazimika
kujitetea kwa wabunge wamwelewe kwamba ni mtetezi wa mamlaka ya Bunge,
isipokuwa ushauri wake umejengwa katika msingi wa Katiba na kanuni.
“Kwa wananchi, wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambao wana kumbukumbu na kinachoendelea hapa nchini wanafahamu juhudi
kubwa nilizofanya mimi mwenyewe kama Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutetea
maslahi ya Bunge hili na mamlaka yake ilipokuwa mamlaka haya yanapingwa
mahakamani lazima tuwe balanced kidogo
wabunge.
“Kwa nafasi yangu, nafasi yangu ni kuwashauri
nimefanya hivyo wananchi wengine wanafahamu, naweza nikataja na hasa yale
mashauri yaliyofanya Bunge hili muhimu likatekeleza wajibu wake kwa ufanisi
wakati baadhi ya wananchi walitaka lisitekeleze wajibu huo. Leo mheshimiwa
Spika baada ya ushauri wangu naomba kiti chako kitupatie mwongozo,"
alisema.
Spika Anne Makinda alisema alipoamua mjadala
ufanyike jana, hakulenga kwamba Serikali iende mahakamani. Alisema sababu ya kusubiri suala hilo
lijadiliwe jana, kwa kuwa watu walikuwa hawafahamu kinachoendelea. Aliruhusu
mjadala kwa kutoa dakika tatu kwa kila
mchangiaji, jambo ambalo pia lilipingwa na hivyo kulazimu atoe dakika 10.
Akihitimisha mjadala wa hoja aliyoiwasilisha
bungeni juzi, Mbatia alishauri kuwepo tume ya kusimamia serikali vizuri kwa
mujibu wa Katiba ili kuona namna ya kufanyia marekebisho sheria kadhaa,
kusaidia Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla.
Mbatia alisema Bunge linahitaji kuangalia upya
sheria ya vyama vya siasa, Sheria ya Haki na Kinga za Bunge Namba 3 ya 1988 na
sheria ya Polisi.
“Na wote kwa pamoja tuombe Bunge lako aidha
liwe na tume, ya kuisimamia serikali vizuri kwa mujibu wa Katiba ili kuweza
kuona ni namna gani sheria hizi zifanyiwe marekebisho haraka ili uchaguzi mkuu
ujao uwe na amani na utulivu na tulisaidie Jeshi la Polisi, tuisaidie serikali
na nchi kwa pamoja,” alisema Mbatia.
Aliongeza kuwa, vipo vitendo vya kihuni ndani
ya Jeshi la Polisi jambo ambalo alitaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta
Jenerali (IGP), Ernest Mangu arejee kwa Saidi Mwema aliyestaafu wadhifa huo
kushauriwa.
Mbunge huyo alimpongeza Spika Anne Makinda kwa
busara zake za kuruhusu mjadala huo na kuonya wabunge kuacha kuingiza siasa
katika suala hilo, kwani wakianza kurushiana maneno, hawatakuwa wanajenga
taifa.
Akizungumza baada ya mjadala huo, Spika
Makinda alisema Kamati ya Bunge ya
Kanuni inatarajia kukaa kuangalia kama kanuni ziko sawa au la. Alitoa mfano wa kanuni ya 47 iliyotumiwa
kujadili suala hilo, Spika Makinda alisema suala hilo lilikuwa kubwa na
halikuwa la dharura kama ambavyo kanuni inatamka.
Awali katika mjadala, wakati baadhi ya wabunge
walilenga kujadili suala hilo kwa misingi ya vyama vyao, Mbunge wa Mkanyageni,
Mohamed Habib Mnyaa (CUF) alionya kulichukulia kivyama.
“Ushauri wangu kwa Bunge, kwa heshima na
taadhima suala hili hata kama ni kweli kwamba CCM inasaidiwa, jambo hili
tusilichukulie kivyama. Najua wabunge wengine wa CCM wameshaumizwa na Jeshi
hili la Polisi,” alisema Mnyaa.
Alishauri, “Naomba Bunge suala hili tulijadili
na tupate maazimio yatakayojenga Jeshi la Polisi katika utaratibu wa kistaarabu
tunakokwenda tusiharibikiwe; Nia ni kujenga.”
Mnyaa ambaye alisema Jeshi la Polisi
limegawanyika, alisema, “Tukiacha jeshi hili, nani anatabiri kitakachotokea
katika uchaguzi ujao. Ni suala la kutofumbia macho.Yako mambo ambayo jeshi
linaonekana limegawanyika. Majambazi wa nchi hii wanatokea ndani ya jeshi. Yako
mambo Jeshi la Polisi lenyewe limegawanyika. Wapo badhi ya polisi wadogo hawana
la kusema wala pa kukimbilia. Bunge liwe kimbilio kwa hawa wanaodhulumiwa”.
Alishutumu kwamba mbali ya kutumia nguvu, polisi
ilitumia silaha zisizowajibika kutumiwa na jeshi, ikiwemo matumizi ya spana ya kutolea tairi kupiga watu vichwani.
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM) alisisitiza kwamba katika jambo lenye maslahi
ya taifa, umoja wa wabunge ni jambo zuri.
“Wapo wanaotaka jambo hili liwe la maslahi ya
kisiasa. Ni kweli CCM imeunda serikali na yanayofanywa na dola si yote ni ya
chama,” alisema. Nkumba ambaye hata hivyo alisisitiza kwamba nchi inaongozwa
kwa sheria na lazima kuwapo utii, alishauri polisi waliohusika katika matumizi
ya nguvu kupita kiasi, wachukuliwe hatua.
“Hakuna mbunge wa kutetea maovu.
Wanaotenganisha wabunge wa CCM na upinzani katika suala la maslahi ya taifa,
watakuwa na ajenda binafsi,” alisema.
Miongoni mwa hoja zilizosababisha wabunge
kugawanyika katika msingi wa kivyama, ni pamoja na iliyotaka Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, wajiuzulu na
kutupia lawama moja kwa moja kwa CCM kwamba ndiyo inayotumiwa na askari
kunyanyasa watu.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
(Chadema) alishutumu Jeshi la Polisi akisema wapinzani wanapigwa na polisi, si
kwa sababu wana makosa, bali wapo mafashisti ndani ya jeshi hilo na serikalini.
Alisema
viongozi wote wa vyama vya siasa, hakuna asiyekuwa na majeraha ya Jeshi la
Polisi na hakuna ambaye hajawahi kukamatwa na kunyanyaswa. “Tuunde tume au
kamati teule kuchunguza mauaji yote, polisi kujeruhi kupiga watu ili tupate
ufumbuzi wa kudumu wa hili suala,” alisema Lissu.
Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamis (CCM)
alisema pamoja na haki ya kuandamana kuwapo, lakini hakuna haki isiyo na
mipaka. “Haki ya kuandamana tusiitumie vibaya tukailaumu Polisi,” alisema
Sadifa ambaye katika mjadala aliiita CUF kuwa ni Saccos, jambo ambalo
Spika Makinda aliamuru aondoe maneno
hayo.
Hata hivyo, Sadifa alianza kugoma kuyaondoa
akimuomba Spika amwamuru pia Lissu aondoe maneno aliyosema CCM ni mafashisti.
Kwa upande wake, Mbunge wa Muhambwe, Felix
Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisema kinachoendelea katika jeshi hilo,
kimekwishafanyiwa uchambuzi na Jumuiya ya Madola kwamba lina mifumo ya
kikoloni, ambayo lengo lake ilikuwa ni kuhakikisha wakoloni wanabaki madarakani
na Waafrika hawaingii madarakani.
Mbunge wa Chwaka, Yahya Kassim Issa (CCM)
alihadharisha akisema si kila aliye ndani ya Serikali ni mwana CCM. Alihoji
kwamba wapo askari wanaouawa lakini wabunge hawawazungumzii. “Nani atatetea
askari katika Bunge hili? Wanakufa hakuna anayewatetea.”
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM)
alisema ni wajibu vyama vyote kulinda amani. Alihadharisha juu ya ushauri wa
kutaka viongozi kujiuzulu akisema lazima kuwa makini na wanaotoa ushauri huo
vinginevyo, viongozi wote wataondolewa madarakani.
No comments:
Post a Comment