Katika
kutekeleza moja ya malengo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa hususan kuwatafutia ajira Watanzania nje ya nchi, Wizara hiyo kupitia
Ubalozi Mdogo wa Tanzania uliopo Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu umefanikisha
kulishawishi Shirika la Ndege la Emirates kuajiri Watanzania wengi zaidi
kuanzia mwaka 2015.
Emirates,
moja ya mashirika ya ndege tajiri zaidi duniani, linamiliki zaidi ya ndege za
kisasa 280, huku likiwa na safari za uhakika duniani kote.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Simba Yahya alisema shirika hilo
litaajiri Watanzania katika kada mbalimbali.
“Wamekubali
kuajiri Watanzania katika kada mbalimbali, ambapo maofisa wake wanaosimamia
ajira watakuja nchini (Tanzania) Machi 2015 kwa ajili ya kuwafanyia usaili
Watanzania watakaoomba kazi hizo na kupata uteuzi wa awali,” alisema.
Aliwataka
Watanzania kuchangamkia ajira hizo, ambazo awali zilitangazwa Julai 2014,
lakini ni Watanzania wachache tu walioomba na hivyo kutofikia lengo
lililokusudiwa.
“Baada
ya mazungumzo ya kina, uongozi wa Emirates umekubali kuongeza muda wa
kuzitangaza ajira hizo kwa mara nyingine na kupanga kufanya usaili kama
ilivyoelekezwa hapo awali,” alisema.
Aliwasisitiza
Watanzania wenye sifa na vigezo stahiki, kutumia fursa hiyo kuomba nafasi hizo
na pia kujiandaa vyema katika usaili ili wajihakikishe ajira katika soko la
ajira la kimataifa.
Kaimu
Mtendaji Mkuu kutoka Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA), Boniface
Chandaruba aliwataka waombaji wote kuhakikisha wanapata barua kutoka wakala
huo.
1 comment:
ajira hizi ni za kujuana tangu nipeleke maombi yangu ubalozini sijapokea hata received confirmation mungu tusaidie vijanawako tunaotafuta ajira hizi maana changamoto za kimaisha ni nyingi.
Post a Comment