Mamlaka ya Maji Safi na Salama Dar es Salaam
(DAWASCO) imewaomba radhi wakazi wa jiji la Dar es Salaam kutokana na
kukosekana kwa huduma ya maji tangu juzi baada ya mtambo wa Ruvu Chini kwenda
Dar es Salaam kupasuka.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika
ofisi za Dawasco, Ofisa Mtendaji Mkuu
Jackson Midala, alisema Ijumaa na Jumamosi mtambo ulizimwa kwa ajili ya
matengenezo na kazi ilikamilika na kuanzia Jumatatu maji yalitoka. Lakini,
alisema kwa bahati mbaya upande mmoja wa mtambo, ulifyatuka na kusababisha
kutopatikana kwa huduma hiyo tangu juzi.
Alisema wamelazimika kuzima mtambo kwa ajili
ya marekebisho na mpaka jana jioni mtambo utakuwa umekamilika na utaendelea
kutoa huduma kama kawaida, hivyo aliwataka wakazi wa jiji kuwa na subira, kwani
mtambo ukizimwa unachukua saa nne hadi tano maji kufika mjini.
“Mtambo ukizimwa maji yanachukua muda kufika,
ila tuna imani kuwa kuanzia alfajiri ya leo maji yatakuwa yamefika na watu
watapata huduma kama kawaida,” alisema Midala.
Aliongeza kuwa maeneo yaliyoathirika na tatizo
hili ni Tegeta, Bagamoyo, Boko, Bunju, Bahari Beach, Sinza, Kinondoni, Sinza,
Mwenge, Chuo Kikuu, Ununio, Masaki, Mwananyamala, Magomeni na Msasani.
No comments:
Post a Comment