Mawakili wa upande wa utetezi katika kesi
mbili za kupokea rushwa ya zaidi ya Sh bilioni 2 kutoka katika akaunti ya
Tegeta Escrow, wameiomba Mahakama kusimamisha kesi hizo hadi itakaposikiliza
hoja zao.
Walidai hayo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, Frank Moshi baada ya washitakiwa
kusomewa upya mashitaka yao.
Washitakiwa hao wanaokabiliwa na kesi mbili
tofauti ni Meneja Misamaha ya Kodi TRA, Kyabukoba Mutabingwa na Mhandisi Mkuu
wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Theophilo Bwakea.
Katika kesi ya Mutabingwa anayedaiwa kupokea
Sh bilioni 2 ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegete
Escrow, Wakili Deo Ringia alidai kuna hoja za kikatiba ambazo zimejitokeza
katika kesi hiyo na zinatakiwa kusikilizwa Mahakama Kuu.
Alidai wamewasilisha notisi ambayo ina nyaraka
watakazozitumia kuishawishi mahakama itoe amri watakazoziomba hivyo aliomba
kesi ipangiwe tarehe ya kutajwa ili Mahakama iangalie hoja hizo na kama
itaridhika isimamishe kesi hadi zitakaposikilizwa.
Hakimu Moshi alisema kesi itatajwa Februari 26
lakini hawatamsomea mshitakiwa maelezo ya awali hadi watakaposikiliza pingamizi
la utetezi kuona kama lina msingi.
Awali akisomewa mashitaka na Wakili kutoka
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) alidaiwa Januari 27,2014
katika benki ya Mkombozi wilaya ya
Ilala, alipokea Sh bilioni 1.6, kutoka kwa
mmiliki wa kampuni ya kufua umeme ya VIP Engineering and Marketing ambaye pia
alikuwa Mkurugenzi wa kampuni ya IPTL, James Rugemalira.
Aidha, anadai Julai 15,2014, alipokea Sh
milioni 161.7, Agosti 26, 2014 Sh milioni 161.7 na Novemba 14, 2014 Sh milioni
161.7, kupitia akaunti namba 00110202613801 kama tuzo kwa kuiwakilisha kampuni
ya Mabibo Beer Winesand Spirits ambayo ni mali ya Rugemalira mahakamani, kitu
ambacho ni kinyume cha sheria.
Anadaiwa kupokea fedha hizo ambazo ni sehemu
ya zile zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow bila kumtaarifu bosi wake
ambaye ni Kamishna wa TRA na kwenye Tume ya Maadili ya viongozi.
Katika kesi ya Bwakea Wakili Ringia aliomba
pia isimamishwe hadi watakaposikiliza hoja zao.
Bwakea anadaiwa, Februari 12, 2014 katika
jengo la Benki ya Mkombozi Ilala alipokea rushwa ya Sh milioni 161,700,000
kutoka kwa Rugemalira akiwa kama mjumbe aliyeandaa sera kuruhusu sekta binafsi
kuzalisha na kuliuzia umeme Shirika la Umeme (Tanesco).
Wakili Swai alidai, Bwakea alijipatia fedha
hizo kupitia akaunti namba 00410102643901 bila kumtaarifu bosi wake ambaye ni
Kamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi. Kesi itatajwa tena Februari 26 mwaka
huu.
No comments:
Post a Comment