ALIYELAWITI MTOTO ATUPWA JELA MIAKA 30


Mahakama ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imemhukumu kifungo cha maisha jela mkazi wa Madibira wilayani hapa kwa kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka mitano.

Aliyehukumiwa kutumikia kifungo hicho ni Samwel Mnyonge (30) ambapo hukumu hiyo imetolewa na hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Mbarali, Guwai Sumaye.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Mazoya Luchagula mbele ya hakimu mfawidhi Sumaye kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Februari 11, 2014 kijijini Madibira.
Alisema awali mshitakiwa alimbeba mtoto huyo wa umri wa miaka mitano kwenye baiskeli akiwa amempa msaada wa kumrejesha nyumbani alipokuwa akitokea shuleni, lakini wakiwa njiani, Mnyonge alimpeleka mtoto kwenye shamba la mahindi na kumlawiti.
Alisema kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata mtoto huyo, alikimbizwa Hospitali ya Mafinga wilayani Mufindi, Iringa na baadaye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam alikotibiwa kwa miezi minane.
Akitoa hukumu baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, Hakimu Mfawidhi Guwai Sumaye alisema anamhukumu Mnyonge kwenda jela kutumikia kifungo cha maisha ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia hiyo.

No comments: