Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck
Sadiki ametaka wazazi kuandikisha watoto
wao katika shule zilizo jirani na maeneo wanayoishi kuwaepusha na usumbufu.
Akizungumza na mwandishi, Sadiki alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya
wazazi kuandikisha watoto wao katika shule mbalimbali zilizopo maeneo ya mbali
na wanapoishi kwa kigezo cha kufuata ubora wa elimu inayotolewa bila kujali
usumbufu wanaopata watoto, ikiwemo suala la usafiri.
Alisema suala hilo linalogeuka kuwa tatizo kwa
watoto kwa kusafiri umbali mrefu, linapaswa kuepukwa na wazazi kwa kuwa yanaweza kumsaidia mtoto kuepuka mambo
mbalimbali wakati anapokwenda au kutoka shuleni.
“Ni vyema wazazi wakazingatia suala hili,
maeneo yote ya jiji hili yana shule nyingi na nzuri kwa ajili ya kuwaandikisha
watoto hawa, umbali siyo mtazamo mzuri kwa kigezo cha kutafuta elimu bora,
suala la msingi ni kuwa karibu na wazazi
katika kufuatilia maendeleo ya mtoto kipindi anapokuwa shuleni,” alisema
Sadiki.
Alisema kuwaandikisha watoto katika shule zilizo mbali na maeneo wanayoishi, kunaweza wakati
mwingine athari zake zisitambuliwe na mzazi kwa haraka kutokana na kutomgusa
moja kwa moja.
Katika hatua nyingine, Sadiki amewataka watumiaji wote wa vyombo vya
usafiri kuwa makini wakati wanavyoviendesha vyombo hivyo kwa lengo la kuepusha
kusababisha madhara yakiwemo ya ajali hususani kipindi hili ambacho shule
nyingi zimeanza kufunguliwa.
Alisema kwa kawaida shule zinapofunguliwa,
watoto wengi huwa barabarani wakati wanapotoka au kwenda shule hivyo ni vyema
kila dereva kwa nafasi yake kuwa makini wakati anapoendesha chombo chake ili
kuhakikisha hasababishi ajali.
Aidha, alionya makondakta pamoja na wapigadebe
juu ya tabia yao ya kuwabughudhi wanafunzi kwa kuwazuia kupanda katika mabasi
na kusisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao pindi
watakapobainika.
No comments:
Post a Comment