VITONGOJI 11 HAVIKUPIGA KURA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA


Wakazi wa vitongoji 11 katika  vijiji vitatu vya  halmashauri ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, wameshindwa kupiga kura kuchagua viongozi wa serikali za vitongoji na vijiji, kutokana nna migogoro ya ardhi iliyopo kwenye vitongoji hivyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero, Azimina Mbilinyi, alisema hayo hivi karibuni mjini hapa.
 Mbilinyi alisema tayari mgogoro hiyo ya ardhi, mashauri yake yamefikishwa katika Mahakama Kuu ya Ardhi.
Alitaja vitongoji hivyo kuwa ni vya kijiji cha  Chiwachiwa Kata ya Mbingu, Miomboni Kata ya Mofu na Idandu kilichopo Kata ya Namawala.
Alisema katika matokeo ya uchaguzi uliofanyika Desemba 14, mwaka huu, CCM wilaya ya Kilombero imeshinda katika viti  vya vijiji 59 sawa na asilimia 55.1,  Chama cha Demorasia na Maendeleo (CHADEMA )  viti 39 sawa na 33.6, Chama cha Wananchi (CUF) vijiji 12 sawa na asilimia 11.2  na  NCCR-Mageuzi hakijashinda hata kiti kimoja.
Kwa upande wa vitongoji , CCM kimepata viti 245 sawa na asilimia 50.6,  CHADEMA viti 190 sawa na asilimia 39.3, CUF viti 48 sawa na asilimia 9.92 na NCCR kiti kimoja  sawa na asilimia mbili.
Watu waliojiandikisha kupiga kura walikuwa ni  143,058  na waliopiga kura walikuwa ni 116,485.

No comments: