Wanawake zaidi ya 200 jana walijitokeza katika kambi ya bure ya uchunguzi wa saratani ya matiti katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi pamoja na kupata ushauri kuhusu saratani ya matiti.
Akizungumza katika kambi
hiyo jana, Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani, Dk Amyn Alidina alisema
hospitali ya Aga Khan inaadhimisha mwezi wa ufahamu wa saratani ya matiti
duniani kwa kutoa huduma ya uchunguzi kwa wanawake bila malipo.
Dk Alidina alisema kambi hiyo ni sehemu ya
kampeni ya hospitali hiyo yenye kaulimbiu “Usisubiri hadi Oktoba” iliyolenga
kuhamasisha umma kuchukua hatua ya kutunza afya zao sasa badala ya kusubiri
muda maalumu wa mwaka.
Dk Alidina alisema
saratani ya matiti inachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo historia ya
saratani katika familia, mfumo wa kazi unaoweza kusababisha kansa, mfumo
wa maisha kama vile uvutaji wa sigara, mfumo wa kula, historia ya maambukizi ya
virusi, na saratani iliyopita.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Mustaafa Bapumia alisema kuwa hospitali
hiyo imeona umuhimu wa kuweka kambi hiyo ili kuwasaidia wanawake baada ya kuona
kwamba tatizo hilo linawakumba wanawake
wengi na wanashindwa kujitambua mapema kutokana na kukosa huduma ya
uchunguzi.
No comments:
Post a Comment