VIFAA VYAKWAMISHA MAFUNZO KWA WANAFUNZI WASIOONA


Upungufu wa vifaa vya kufundishia katika Shule ya Sekondari ya Wasioona ya Mvumi DCT iliyopo katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma unawakwamisha wanafunzi wasioona kufuata vyema na kwa wakati mtaala wa masomo.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na  Mwalimu Mtaalamu wa shule ya wasioona ya Mvumi DCT, Ernest Mbilu wakati wa ziara ya Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing.
Alisema  shule hiyo ina wanafunzi 31 wasioona ambapo wavulana ni 18 na wasichana ni 13 lakini wanafunzi hao wamekuwa wakichanganywa na wasioona..
Alisema watoto wenye ulemavu wa kutoona wanahitaji kufundishwa kwa kutumia vifaa maalumu ili waweze kwenda sambamba na wale wanaoona lakini upungufu wa vifaa vya kufundishia wanafunzi wasiiona imekuwa ni kikwazo kikubwa.
Pia mwalimu huyo alisema kama vifaa vya kufundishia wanafunzi wasioona vitapatikana wanafunzi hao watafanya vizuri zaidi katika masomo yao tofauti na sasa ambapo wamekuwa wakiachwa nyuma.
Akizungumza na wanafunzi hao Balozi Youqing aliwataka kujifunza kwa bidii.
“Leo mko darasani lakini kesho mtakuwa kwenye ujenzi wa nchi na mkitaka kuwa wataalam na kupata maisha mazuri lazima kujifunza na kufanya kazi kwa bidii” alisema
Pia balozi huyo alisema Serikali ya China imetoa  fedha kwa ajili ya kusaidia shule hiyo na kati ya Sh milioni 50 zilizotolewa kusaidia elimu katika Wilaya ya Chamwino, shule ya Mvumi wasioona DCT itapata sehemu yake katika fedha hizo.
Aidha balozi huyo alishiriki ujenzi wa maabara kwenye shule ya sekondari ya Mvumi.
Alisema Tanzania ina raslimali nyingi ni vizuri kama watu wake wakaelimika na kupata ujuzi mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa Taifa.
 Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Fatma Ally alisema wilaya hiyo inatakiwa kujenga vyumba 81 vya maabara.
 Alisema awali walitakiwa kukabidhi maabara hizo Novemba 15, mwaka huu lakini baada ya kauli ya Rais Jakaya Kikwete kutaka kila shule kuwa na vyumba vitatu vya maabara ana uhakika ifikapo Desemba 10, mwaka huu kazi hiyo itakuwa tayari.
 Alisema sasa vyumba vinne vya maabara vimekamilika, vyumba 25 viko katika hatua mbalimbali lakini mpaka Desemba 10 watakuwa wamekamilisha agizo la Rais Kikwete.

No comments: