WANAFUNZI WAPEWA MAFUNZO YA MATUMIZI BORA YA FEDHA



Benki ya Barclays tawi la Iringa imetoa mafunzo ya utunzaji wa fedha kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Highlands ya mjini hapa waliokiri matumizi ya pombe yanazifanya baadhi ya familia zao kukosa akiba.
Katika majadiliano yao, wanafunzi hao walitaja vipaumbele vya familia zao kwamba ni malazi, chakula, maji, shule na mavazi hata hivyo wakasema pamoja na umuhimu wake, matumizi ya pombe na vitu vingine vya anasa yanadhohofisha upatikanaji wa huduma hizo kwa sababu ya kukosa akiba. 
Meneja wa tawi hilo, Shamsa Abdulatif alisema katika mafunzo hayo yanayotarajiwa kuwanufaisha wanafunzi wa shule nyingine za mkoani hapa kwamba, kila mtu anaweza kufikia ndoto ya mahitaji yake kama atakuwa na nidhamu ya matumizi sahihi ya fedha.
Aliyataja mahitaji hayo kuwa ni pamoja na kumudu gharama za elimu, ujenzi, ununuzi wa vyombo mbalimbali vya usafiri, vyakula na huduma nyingine muhimu kwa matumizi ya binadamu.
“Wanafunzi mnaweza kujiwekea akiba kutokana na kidogo mnachopewa na wazazi wenu kwa ajili ya matumizi yenu ya kila siku muwapo shuleni, lakini pia mnaweza kusaidia kuwashauri wazazi na walezi wenu kujiepusha na matumizi yasio ya lazima ili mpate akiba,” alisema.
Meneja huyo alitoa mfano akisema katika kila Sh 1,000 anayopewa mwanafunzi kwa ajili ya matumizi yake shuleni anaweza kujiwekea akiba ya hadi nusu ya kiasi hicho ambacho kwa mwaka kinaweza kuwa kikubwa.

No comments: