MAONESHO YA BIASHARA YA TIBA ASILI YA MWAFRIKA YAJA



Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Tiba Asili ya Mwafrika yatakayofanyika kuanzia Novemba 16, mwaka huu kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Maonesho hayo yatakayofanyika nchini kwa mara ya kwanza yameandaliwa na Jukwaa la Tiba Asili Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade).
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maonesho hayo, Boniventure Mwalongo, wadau mbalimbali wa tiba asili na tiba mbadala wanatarajia kushiriki katika Maonesho hayo.
Mwalongo alisema washiriki hao ni pamoja na watabibu wa tiba asili, watengenezaji wa dawa asili, wakunga wa  tiba asili,  kampuni za dawa asili na vipodozi vya dawa asili, wasambazaji wa tiba asili na tiba mbadala, watengenezaji wa vyakula asili, kliniki za tiba asili na tiba mbadala.
Aidha, Mwalongo alisema wanaendelea na taratibu za kufanya maongezi na wadhamini mbalimbali ambapo watatoa taarifa rasmi baada ya kufikia tamati ya maongezi, ikiwa ni pamoja na kutoa ratiba nzima ya maonesho hayo. Wadau wasiopungua 280  wameonesha nia ya kushiriki.

No comments: