WATETEA VIONGOZI KUFUNGUA AKAUNTI NJE YA NCHI


Baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wametetea viongozi kufungua akaunti nje ya nchi wakisema uongozi si utumwa. 
Wajumbe Charles Mwijage (pichani)  na Jasson Rweikiza walisema kuwakataza wasifanye hivyo, kumepitwa na wakati. 
Hata hivyo kwa upande wake, mjumbe Nyambari  Nyangwine  alisema kuruhusiwa viongozi kufungua akaunti nje ni kuwaruhusu waibe rasilimali zao. 
Nyangwine alihoji wanaoenda kufungua akaunti nje ya nchi wanaficha jambo gani. 
Hoja hiyo iliungwa mkono na Zainab Gama ambaye alisema Katiba ikiruhusu jambo hilo viongozi wengi watapata fursa ya kutorosha rasilimali za nchi kuzipeleka nje. 
Gama pia alisisitiza taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) iingizwe kwenye Katiba akisema nchi na wananchi wake wameteswa na tatizo la rushwa. 
Alisema Takukuru imeshindwa kushughulikia rushwa wakati wa uchaguzi kwa sababu sheria zilizopo haziwapi nguvu ya kufanya kazi hiyo. 
“Kama kuna kiongozi anapinga Takukuru kuingizwa kwenye Katiba, huyo nina wasiwasi naye juu ya uadilifu wake,” alisema Gama. 
Eneo lingine lililochangiwa ni kuhusu Makamu wa Rais; ambalo wajumbe wameendelea kutofautiana namna gani msaidizi huyo wa Rais apatikane chini ya mfumo wa serikali mbili. 
Mapendekezo ya wajumbe hao  yaliendelea kutofautiana kwani wapo waliotaka kuwepo na makamu watatu. Kati ya hao mmoja awe mgombea mwenza lakini Katiba iwatambue rais wa Zanzibar naye awe makamu wa rais ili kupata hadhi ya kimataifa wakati waziri mkuu naye apewe hadhi hiyo.

No comments: