SUALA LA URAIA PACHA BADO 'JIWE GUMU' BUNGE MAALUMU


Uraia pacha kwa Watanzania walioko nje ya nchi jana uliendelea kutawala katika mijadala kwenye Bunge la Katiba huku wengi waliochangia wakikubaliana wasio na uraia Katiba iruhusu wapewe chini ya utaratibu wa uraia wa pacha. 
Wachangiaji  wengi  walisema hakuna sababu ya kuwanyima uraia hao kwa kisingizio kuwa sio wazalendo. 
Selemani Ali alisema Watanzania walioenda nje ya nchi kusaka maisha umefika wakati warejeshewe uraia wao kwani watapata fursa pia ya kufaidika na matunda ya nchi yao. 
Lakini Luis Majaliwa alisema Watanzania hao hawana hadhi ya kupewa uraia kwa sababu si wazalendo kwani walikimbia nchi kwa kuona maisha ni magumu na kuwaacha wenzao wanahangaika kuikwamua nchi kwenye maendeleo. 
Alisema, “iweje leo hii walioacha jahazi linazama waona mambo yanaenda vizuri waruhusiwe kuja kupewa tena uraia.” Alipendekeza  Katiba isiwape hadhi ya kupewa uraia. 
Mjumbe Nyambali Nyangwine alisema Katiba isiweke masharti magumu kwa Watanzania walioko nje ambao wanataka kupata uraia wa nchini. 
Alisema umefika wakati wa Watanzania kubadilisha fikra na msimamo na mitizamo yao dhidi ya Watanzania walioko nje ya nchi. 
Zakia Meghji  alisema walioko nje ya nchi ni Watanzania na wanafanya kazi na sehemu ya fedha hizo wanazituma kwa jamii zao zilizoko nchini na wanaweza kuja kuwekeza pia nchini. 
Alisema hakuna sababu ya kuwakatalia kuwapa uraia kwani walikana uraia wa hapa nchini ili waweze kufaidika na elimu ya nje pamoja kupata ajira. 
“Hapa tunatoa uraia kwa watu ambao siyo Watanzania, iweje tuwanyime watoto wetu uraia?” Alihoji Meghji. 
Mussa Azzan Zungu  alisema haoni sababu inayokera Watanzania hadi wawanyime Watanzania wenzao walioko nje kupatiwa uraia. 
Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Jasson Rweikiza ambaye alisema umefika wakati watu waachwe wawe na uraia wa nchi mbili ili kutoa fursa zaidi kwa vijana wa kitanzania kwenda nje kusaka maisha. 
Ave Maria Semakafu alisema Watanzania hao walioko nje walienda huko kusaka ajira kutokana na tatizo la ajira lililoko hapa  nchini na akahoji wakirudi wote hao ajira zitapatikana wapi? 
Alishauri mfumo wa kuwapatia uraia ukubaliwe kwani kwenda kwao nje ya nchi sio kwamba walikosa uzalendo ila walienda kusaka maisha zaidi. 
Zainabu Gama naye alikubaliana na hoja hiyo na akasema kwamba kuwanyima uraia Watanzania hao ni kuwaonea.

No comments: