TAREHE ZA MWISHO WA BUNGE LA KATIBA ZAPISHANA


Kutokana na kalenda ya Bunge Maalumu la Katiba kutofautiana na ile ya Serikali kuhusu lini Bunge hilo  litamalizika, Kamati ya Uongozi imelazimika kuiagiza Sekretarieti ya Bunge hilo kufuatilia serikalini kujua kwa nini kumekuwepo na tofauti hizo. 
Wakati tamko la Serikali linaonesha kuwa Bunge hilo linatakiwa kumalizika Oktoba 4 mwaka huu, kalenda ya Bunge hilo ambayo wamegawiwa wajumbe inaonesha kuwa Bunge hilo litamalizika mwishoni mwa mwezi Oktoba. 
Hali hiyo ilifanya mjumbe wa Bunge hilo Ezekiah Olouch mwishoni mwa wiki kuomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge  hilo kutaka kujua sababu ya tofauti hizo kubwa jambo ambalo linaweza kuathiri utendaji wa Bunge hilo. 
“Mheshimiwa naomba mwongozo wa jambo hili, kalenda ya shughuli za Bunge hili ambalo mmetupatia sisi wajumbe inaonesha kuwa litamalizika mwishoni mwa Oktoba, lakini tamko la Serikali ambalo limechapishwa na gazeti la Serikali linaonesha Bunge hili litamalizika mwanzoni mwa Oktoba. 
“Katika tofauti hizi tufuate lipi, huoni kwamba shughuli za Bunge hilo zitavurugika kutokana na kalenda hii mliyotupa wakati Serikali ina kalenda yake ya kumalizika kwa Bunge? Alihoji na kuomba mwongozo wa Mwenyekiti. 
Makamu Mwenyekiti Samia Suluhu wakati akitoa mwongozo wake juzi jioni, alisema suala hilo tayari Kamati ya Uongozi imeliona na imemwagiza Katibu wa Bunge afuatilie jambo hilo kwa kina huko serikalini. 
“Tangu Septemba 2 kamati ya uongozi tulipokaa suala hilo tuliliona na tayari tumemwagiza Katibu wa Bunge alifuatilie na tutatoa taarifa hapa bungeni,” alisema Suluhu.

No comments: