MTOTO AKIMBIA NYUMBANI KWA ADHABU ZILIZOPITILIZAMtoto mmoja mkazi wa wilayani Bunda mkoani Mara, amelazimika kukimbia kwao na kwenda kwenye nyumba ya mtu mwingine katika mtaa mwingine, kukwepa viboko.
Imedaiwa  kuwa baba yake mzazi mtoto huyo  alikuwa akimcharaza viboko mwanawe kwa kutumia mijeledi na mipira, na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miaka 9 anayesoma darasa la tatu katika shule ya msingi Balili iliyoko mjini Bunda, (jina limelihifadhiwa) anayeishi na baba yake, Stephen Nyamusarya, baada ya mama yao kudaiwa kuwatelekeza kutokana na kile kinachodaiwa ni kipigo kutoka kwa baba yao, alikimbilia kwa mwananchi huyo anayeishi katika mtaa wa idara ya Maji juzi saa 1:30 usiku.
Msamaria huyo Yehoyada Keheri, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Bigutu, alimchukua mtoto huyo na kumpeleka polisi baada ya kushuhudia akiwa na majeraha makubwa katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Alisema baada ya kufika polisi alitakiwa afungue jalada na kisha akaombwa aendelee kukaa na mtoto huyo huku taratibu za kumpeleka kwenye kituo cha kulea watoto kilichoko mjini Musoma zikifanyika.
Kwa upande wake mtoto huyo alipohojiwa na gazeti hili, alisema kuwa baba yake huyo amekuwa akifika nyumbani akiwa amelewa na kuanza kumcharaza viboko kwa kutumia mijeledi na mipira huku akiwa amemfunga miguu na mikono kwenye mti.
Jeshi la polisi katika wilaya ya Bunda, limethibitisha kesi hiyo kufunguliwa kwa namba  BND/RB/4105/2014 na kwamba wanamsaka mtuhumiwa huyo ili aweze kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili ya shambulio la kuzuru mwili.

No comments: