Mazungumzo kati ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa vyama
vya siasa, yamefanyika vizuri katika Ikulu ndogo ya Dodoma na kufikia
makubaliano katika baadhi ya maeneo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo
jana, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD), John Cheyo, alisema mazungumzo
yameendelea kuwa mazuri na mara hii wamefikia makubaliano katika baadhi ya
mambo.
“Mazungumzo yalikuwa mazuri na kuna baadhi ya maeneo
tumekubaliana, lakini taarifa zaidi tutaitoa kesho kwenye mkutano na waandishi
wa habari,” alisema Cheyo.
Mkutano huo ambao ni wa pili kati ya Rais Kikwete na
viongozi wa vyama hivyo, ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa vyama vya CCM, Chama
cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na
NCCR-Mageuzi, ambavyo vinaunda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Viongozi wengine waliohudhuria ni kutoka Tanzania Labour
Party (TLP) na United Democratic Party (UDP) na vyama vingine visivyo na
wabunge, viliwakilishwa na chama cha UPDP.
Kwa upande wa CCM, waliohudhuria mkutano ni Katibu Mkuu,
Abdulrahman Kinana na Makamu Mwenyekiti, Philip Mangula; Chadema iliwakilishwa
na Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wake, Tundu Lissu.
CUF iliwakilishwa Mwenyekiti wa Taifa, Profesa Ibrahimu
Lipumba wakati NCCR-Mageuzi iliwakilishwa na Mwenyekiti wa Taifa, James Mbatia.
TLP iliwakilishwa na Mwenyekiti wake wa Taifa, Augustine Mrema wakati Fahmi
Dovutwa wa UPDP aliwakilisha vyama vingine visivyo na wabunge.
Mbali na Cheyo kusema kuwa kuna baadhi ya mambo kimsingi
wamekubaliana, hakuna kiongozi hata
mmoja ambaye alikuwa tayari kusema mambo waliyokubaliana hadharani, zaidi
ya Mrema kujipigia debe kuwa ameendelea kumsemea Mbatia kwa Rais, kutokana na
kitendo chake cha kunyatia jimbo la Vunjo.
“Nimemkumbusha tena Rais suala la Mbatia na Rais kamwambia
Mbatia kuwa amemteua ili aende bungeni na sio aende Vunjo,” Mrema aliwaambia
waandishi wa habari nje ya hoteli ya Dodoma, ambako wajumbe hao walikutana kwa
muda baada ya kutoka Ikulu ndogo ya Dodoma.
Mazungumzo ya viongozi hao wa kisiasa, yana lengo la
kutafuta muafaka wa mchakato wa Katiba, ambao umesuswa na Ukawa, ambao wanadai
kuwa Bunge Maalumu la Katiba, halina mamlaka ya kubadili baadhi ya vifungu
katika Rasimu ya Katiba mpya, iliyotengenezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba
mpya.
Baada ya Ukawa kususa na kutoka nje ya Bunge hilo, wamekuwa
wakimtaka Rais Kikwete avunje Bunge Maalumu, kwa madai kuwa limekosa uhalali wa
kisiasa, baada ya vyama vinavyounda umoja huo kusisitiza kuendelea kususa.
Hata hivyo, tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick
Werema, aliweka wazi kuwa Sheria iliyoanzisha mchakato huo na kuunda Bunge
hilo, haikutoa mwanya wa mtu yeyote kuvunja bunge hilo.
Badala yake, sheria imempa mamlaka Rais kuongeza siku za
kufanya vikao vya Bunge hilo, iwapo litakuwa halijamaliza kuandika Katiba mpya
ndani ya siku 70.
Wananchi wengi wana hamu ya kusikia yaliyojiri ndani ya
kikao hicho, kutokana na unyeti wa jambo lenyewe la Katiba. Cheyo aliahidi
kukata kiu hiyo ya Watanzania leo mchana, atakapozungumza na wanahabari mjini
hapa.
No comments:
Post a Comment