Watu wanane wamekufa papo hapo na wengine 11 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria jana kuacha njia na kupinduka katika Mlima Katete kijijini Milumba wilayani Mlele.
Akizungumza na mwandishi kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema ajali hiyo iliyotokea saa 11 alfajiri ilihusisha lori aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 234 AXK.
Aliongeza kuwa gari hilo likiwa limesheni bidhaa mbalimbali lilikuwa likitokea kijiji cha Kibaoni wilayani Mlele likielekea mjini Sumbawanga mkoani Rukwa likiwa linaendeshwa na Jamal Mohammed (42) Mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam.
Kamanda Kidavashari amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Peter Lusambo (24), Ngelela Shauritanga (29), John Pius (32). Mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja tu la Linus (30) wote wakiwa wakazi wa kijiji cha Kibaoni Wilaya ya Mlele.
Aliwataja wengine kuwa ni pamoja na Makono Kisumu (23), Elias Mussa (28) wakazi wa wilaya ya Geita Mwanza, Ally (34) mkazi wa Dar es Salaam ambaye alikuwa utingo wa gari hilo na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Abbas (28), mkazi wa Mtaa wa Mpanda Hoteli wilayani Mpanda .
Majeruhi ambao wamelazwa kwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ni pamoja na Kaswagula Linus (25), Peter Mkalala ( 30), Peter Lusambo (20) Castory Kaombwe (23) Nassor Ramadhan (22) wote wakiwa wakazi wa Kata ya Kibaoni Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi. Wengine ni Salim Hassan (42) mkazi wa mjini Mwanza, Jamari Mohamed (42) Salumu Njomoke (22) wakazi wa Dar es Salaam na John Chambaneje (32) mkazi wa Mtaa wa Mpanda Hoteli mjini Mpanda.
Kamanda Kidavashari alisema chanzo cha ajali hiyo ni kukatika kwa chombo aina ya propela, hivyo kumshinda dereva wa gari hilo na kupinduka.
Kwa mujibu wa Kidavashari dereva wa gari hilo amekamatwa na jeshi la Polisi ambapo anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali kukamilika.
No comments:
Post a Comment