Wilaya ya Ilala
imeanzisha kampeni ya wiki tatu ya usafi
katika maeneo yaliyopo katikati ya jiji la Dar es Salaam kwa lengo la
kutoa elimu na kuyaweka maeneo hayo safi na salama.
Kampeni
hiyo ilizinduliwa jana katika eneo la Kisutu na Mkuu wa wilaya ya Ilala Raymond
Mushi.
Akizindua
kampeni hiyo alisema bila suala la usafi
kufanyiwa kazi, wageni wataona kwamba mambo katika Jiji la Dar es Salaam ni
hovyo hasa ikizingatiwa kwamba katikati ya Jiji ndio sebule ya Jiji.
Kampeni
hiyo inayosimamiwa na kampuni yenye dhamana ya usafi katika eneo hilo la kati
ya Green Waste Pro Limited inashirikisha wananchi kwa lengo la kuwafanya wawe
washirika wa usafi kwa kujenga utamaduni wa kuchukia uchafu.
Mkuu
huyo wa Wilaya pamoja na kushukuru wananchi na wanafunzi wa Shule ya Kisutu
waliofika katika kampeni aliwataka
viongozi kujipanga kuhakikisha kampeni hiyo inakuwa endelevu na yenye
mafanikio.
Kampeni
hiyo inafanyika katika Kata ya Kivukoni, Kisutu na Mchafukoge.
Pamoja
na Mkuu huyo wa Wilaya kusema kwamba kampeni hiyo ni chachu kwa kata za
pembezoni za kujali usafi amewataka
wananchi kuwa washiriki kwa kuhakikisha hawatupi uchafu hovyo.
Naye
Naibu Meya na Diwani wa Kisutu Kheri Kessy alisema kazi ya usafi inakabiliwa na
changamoto kubwa hasa kutokana na kuvuja kwa chemba za maji machafu na wananchi
kutupa taka hovyo.
Alisema
wananchi na hasa wapitanjia kama
wakijifunza kutupa uchafu maeneo wanayotakiwa watakuwa wamesaidia sana kujenga
utamaduni wa kuchukia uchafu na pia kufanya maeneo yapendeze.
Alisema
wananchi wa Kata yake ya Kisutu ni waelewa tangu kuanza kwa kampeni hizo miaka
miwili iliyopita lakini wapitanjia wamekuwa wakivuruga utaratibu wa usafi.
Aliwataka
wakazi wa Dar es Salaam kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha hawatupi taka hovyo
na kuanza kuuchukia uchafu kutoka katika majumba yao hadi wanakotembea.
Kampuni inayoendesha kampeni hiyo ya Green Waste kupitia
kwa Meneja wao Abdallah Mbena amesema kwamba kuna maendeleo makubwa katika
kampeni za kuweka Jiji safi na safari hii wamewaalika wenzao kutoka Segerea na
Upanga ili waone njia wanazotumia kuweka maeneo yao yenye dhamana safi na ya
kupendeza.
Mbena alisema changamoto kubwa zinazokabili juhudi za kuweka maeneo safi ni
upungufu wa usimamizi katika sheria kwani wengi hawakubali kuzitii.
Alisema kama wangezitii kungekuwa na usafi kila siku. Kwani wengine
wamekuwa wakifika katika majengo yao na kuyasafisha na kutupa uchafu barabarani
wakati wafagiaji wameshafanyakazi yao usiku.
No comments:
Post a Comment