WIZARA YAHOFU TAARIFA POTOFU ZA EBOLA KUKIMBIZA WATALII

Wizara ya Maliasili na Utalii imetaka ufanyike utafiti wa kina  ukiambatana na utoaji taarifa sahihi kuhusu ugonjwa wa ebola  kuepuka kupotosha na kusababisha watalii kuhofu kuingia nchini.
Mkurugenzi wa Utalii, Zahoro Kimwaga aliyasema hayo jana wakati wa Mkutano wa Kamati ya Huduma za Watalii (TFC) uliolenga kupata michango kukabili changamoto mbalimbali.
Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi alimuunga mkono mkurugenzi huyo na kuwahakikishia watalii kwamba ugonjwa huo hauko nchini na kwamba serikali imejiandaa vizuri kuukabili.
“Ili kukabiliana na suala ugonjwa huo ni vema utafiti wa kina ukafanywa nchini na kutolewa taarifa sahihi huku kukiwa na hatua madhubuti kukabiliana na ugonjwa huo, lakini pia kuwaondolea hofu watalii wanaotaka kuingia nchini,” alisema.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amesema serikali imejipanga baada ya miaka mitatu  kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini kufikia milioni 2.3.
Hatua hiyo inakwenda sambamba na kuboresha masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utoaji huduma ambao unalalamikiwa na watalii wengi na pia kuboresha ulinzi na usalama. Tarishi alisema mwaka jana Tanzania ilipokea watalii milioni 1.1.
Akizungumzia ulinzi na usalama kwa watalii, Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa wanadiplomasia na Watalii, Benedict Kitarike alisema matendo ya kuvamiwa kwa watalii nchini yamekuwa yakipungua kila mwaka.

No comments: