Serikali imeandaa sera ya petroli itakayowezesha asilimia tatu ya mapato yatakayopatikana kutokana na uchimbaji wa rasilimali hiyo kubaki katika halmashauri ya eneo hilo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Mjiolojia Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Adam Zuberi alisema hatua hiyo ni kuhakikisha rasilimali hiyo inanufaisha Watanzania wote ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha katika hatua ya utekelezaji wake.
Alisema hayo jana wakati wa kongamano la wadau kujadili sera ya petroli iliyowashirikisha viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, taasisi zisizo za kiserikali na wadau mbalimbali wa masuala hayo ili kutoa mapendekezo zaidi katika sera hiyo.
Alisema pia sera hiyo itasaidia kuwawezesha watanzania kushiriki katika utafutaji wa mafuta kwa kushirikiana na makampuni ya nje kwa kupata wataalamu wenye taknolojia hizo.
Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alisema kongamano hilo litapata michango ya wadau ili sera hiyo isadie rasilimali ya Watanzania iwanufaishe kwa kutengeneza sheria na kanuni.
Alisema katika miaka 17 iliyopita kuanzia mwaka 1997 hadi 2014, Serikali imesaini mikataba 26 ya utafutaji na uzalishaji mafuta ambapo mikataba iliyosainiwa ni ugunduzi wa gesi asilia katika maeneo 19 nchini.
Kandoro alisema kati ya maeneo hayo matano yapo katika maeneo ya mwambao na maeneo 14 yako katika kina kirefu cha maji ya baharini ambapo hadi kufikia Julai, 2014 kiasi cha gesi iliyogunduliwa nchini inakariba futi za ujazo trilioni 50.5
Alisema ukuaji wa haraka wa sekta ndogo ya utafutaji na uzalishaji mafuta kumefanya Serikali kuona umuhimu wa kuandaa sera ya petroli itakayotoa miongozo mahsusi ya kusimamia kwa ufanisi shughuli za utafutaji na uzalishaji mafuta na gesi asilia na kuendesha biashara ya mafuta ikiwemo usafirishaji, usambazaji na matumizi ya petroli nchini.
Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Askofu David Mwasota aliunga mkono suala la uwazi katika sera hiyo, kwa kuwashirikisha wadau na kutaka mapato yanufaishe Watanzania wote.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Lipumba alisema ni vema mikataba yote iwekwe wazi kwa lengo la kuhakikisha zinafuata sera zilizotungwa kwa manufaa ya Watanzania wote.
No comments:
Post a Comment