KKKT WATAKA KATIBA YA WATANZANIA


Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kikristo Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma Mchungaji Samweli Mshana, amewataka wajumbe walio katika mchakato wa Katiba kuhakikisha wanawapatia watanzania Katiba itakayotoa haki zote bila upendeleo. 
Aidha, alisema kanisa hilo halitarajii Katiba hiyo kumilikiwa na vyama vya siasa na viongozi wao au kuwa ya kiitikadi. 
Mchungaji Mshana alisema hayo akizungumza katika tamasha la akinamama KKKT Jimbo la Makao Makuu, Dodoma. 
Mchungaji huyo alisema hatarajii kuona wajumbe hao wakijadili Katiba kwa kupendelea upande wowote ule wa jamii. 
Naye Mwenyekiti wa Wanawake Jimbo la Makao Makuu KKKT Dodoma, Salome Kingu alisema wanawake wa jimbo hilo tangu lianze Bunge hilo la Katiba wamekuwa wakimlilia Mungu ili Katiba iweze kuwa ya Watanzania wote na itakayojali haki. 
Katika tamasha hilo mafundisho mbalimbali yatafundishwa ikiwemo somo la Maadili ya Mwanamke katika kanisa na Ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia kwa wakati huu tulionao na somo la Maadili ya Wanawake, Sheria na Mirathi.

No comments: